Ingawa Wabunge wa baraza la wawakilishi wameidhinisha mswada wa bajeti ya muda Jumanne jioni kufuatana na misimamo ya vyama vyao lakini kazi kubwa itakua katika baraza la Senate ambako kura 60 zinahitajika kuidhinisha mswada huo.
Wabunge 245 wa chama cha Republican walipitisha mswada wa matumizi ya serikali huku wa-Democrat wakipinga kwa kura 182 ikwa ni muda mfupi tu baada ya Rais Donald Trump kusema angependa kuona serikali kuu imefungwa.
Baraza la wawakilishi likiongozwa na warepublican kwa hivyo wamepeleka mswada huo kwa baraza la seneti ikiwa ni mswada wa tano wa mwaka huu tangu mwezi Oktoba ili kuruhusu serikali kufanya kazi hadi Marchi 23.
Mswada huo haujapendekeza mageuzi katika mfumo wa uhamiaji suala lililosababisha kukwama kwa kura ya mwezi uliopita na kupelekea serikali kuu kufungwa kwa siku tatu.
Baraza la senate linatazamiwa kupigia kura mswada huo baadae Jumatano ambapo baadhi ya maseneta wakisema kuna maendeleo yanayopatikana lakini mvutano uliopo ni kwamba warepublican wanataka kuongeza matumizi ya jeshi huku wademocrat wanataka matumizi ya huduma za afya na maswala ya kijamii yapewe kipaumbele.
Rais Trump na wabunge wa chama cha Republican kwa upande wao wanataka mageuzi ya uhamiaji yaambatanishwe na kuidhinishwa kwa bajeti ya mwaka huu.