Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Januari 20, 2025 Local time: 23:53

Ruto akosoa vikali waendesha mashtaka wa ICC


Naibu Rais wa Kenya, William Ruto katika hoteli ya Movenpick,The Hague,Uholanzi, Oct.15, 2013.
Naibu Rais wa Kenya, William Ruto katika hoteli ya Movenpick,The Hague,Uholanzi, Oct.15, 2013.
Naibu Rais wa Kenya William Ruto amewaambia waandishi wa habari huko The Hague anakohudhuria vikao vya kesi dhidi yake kuwa ataendelea kuhudhuria vikao hivyo huku Kenya ikisubiri maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa maamuzi juu ya kuahirishwa kwa kesi dhidi yake na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne huko Uholanzi, bwana Ruto alitumia maneno makali dhidi ya waendesha mashtaka wa mahakama ya ICC akisema imebainika wazi kuwa utendaji kazi wao ulikuwa hovyo na kwamba waliwashawishi mashahidi kwa kuwapa hongo ili kutoa ushahidi wa uwongo dhidi yake na washtakiwa wenzake.

Alisema pia kuwa yeye na Rais wa Kenya wanaitaka mahakama hiyo kuheshimu sheria za Kenya na kuwaruhusu kuhudumia taifa lao kama viongozi waliochaguliwa kihalali na wananchi na hivyo kuzisikiliza kesi hizo kwa muda uliotengwa na sio mfululizo ili kuwe na mizani ya kikazi upande wao kama viongozi na upande wa waendesha mashtaka.

Aidha bwana Ruto amesema yeye na Rais Kenyatta wanasubiri maamuzi ya baraza hilo la usalama kuahirisha kesi dhidi yao kama ilivyoombwa rasmi na serikali.

Mwishoni mwa wiki viongozi wa Umoja wa Afrika katika mkutano maalum mjini Addis Ababa, Ethiopia walitoa mwito kwa Baraza la Usalama kufikia azimio litakaloahirisha kwa mwaka mmoja kesi dhidi ya viongozi hao wa Kenya.

Viongozi hao wa Afrika walimshauri Rais Kenyatta kutohudhuria vikao vya kesi dhidi yake vinavyotarajiwa kuanza Novemba 12 huko The Hague katika mahakama ya kimataifa –ICC.
XS
SM
MD
LG