Harris ambaye aliwahi kuwa mwendesha mashitaka alisema katika mkutano wa usalama mjini Munich kwamba wamekusanya ushahidi wa kutosha pamoja na kufahamu viwango vya kisheria, na kwa hivyo hawana shaka kwamba ukatili dhidi ya ubinadamu umetekelezwa.
Ameongeza kusema kwamba wale wote walioshiriki kwenye ukatili huo , pamoja na viongozi waliowaamuru watawajibishwa kwa mujibu wa sheria. Matamshi ya Harris yamekuja wakati viongozi wa mataifa ya magharibi wanakutana mjini humo ili kutathimini kuhusu vita hivyo vibaya zaidi barani Ulaya tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.
Washington inatumai kwamba itaweza kumtenga zaidi Rais wa Russia Vladimir Putin, pamoja na kuchukua hatua za kisheria, ili kuwawajibisha maafisa wa serikali, yake kupitia vikwazo pamoja na mahakama za kimataifa. Wakati huo huo rais wa Ukraine Volodymr Zelenskiyy wakati akihutubia mkutano huo wa Munich kwa njia ya video amesema kwamba hakuna njia nyingine ila ushindi wa taifa lake kwenye mapigano hayo. Amesema kwamba kila mara Russia inalenga silaha dhidi ya Ukraine, ni sawa na kuielekeza kwa jirani zake.