Russia iliishambulia Ukraine kwa makombora siku ya Alhamisi ikiwa ni pamoja na yale yaliyoulenga mji mkuu wa Kyiv pamoja na mji kaskazini mashariki wa Kharkiv.
Jeshi la Ukraine limesema limepiga makombora 54 kati ya 69 yaliyorushwa na Russia.
"Unyama usio na maana. Haya ndiyo maneno pekee yanayoingia akilini kuona Russia ikirusha makombora mengine katika miji ya amani ya Ukraine kabla ya mwaka mpya," Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter. "Haiwezekani 'kutoegemea upande wowote' mbele ya uhalifu mkubwa kama huo wa kivita. Kujifanya 'kutoegemea upande wowote' ni sawa na kuchukua upande wa Russia."
Shambulio hilo lilisababisha ving'ora vya uvamizi wa anga kote nchini, na maafisa wa Ukraine walisema mifumo ya ulinzi wa anga iliweza kuangusha makombora yanayoingia.
Meya wa Kharkiv Ihor Terekhov aliripoti milipuko katika mji wake na kusema mamlaka zinabaini kilichopigwa na iwapo kulikuwa na majeruhi wowote.