Akufo Addo wiki iliyopita alizua mtafaruku baada ya kudai kwamba Burkina Faso iliajiri mamluki kutoka kundi la Wagner la Russia, ili kusaidia kwenye mapambano dhidi ya wanamgambo wa kiislamu.
Wakati akizungumza na wanahabari akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Akufo Addo alisema kwamba anaamini mgodi uliyopo kusini mwa Burkina Faso umepewa mamluki hao kama njia ya malipo kwa huduma zao.
Serikali ya Burkina Faso haijakanusha wala kukubali madai hayo, ingawa imemuita balozi wa Ghana nchini humo kwa mkutano siku ya Ijumaa, ili afafanue zaidi kuhusu matamshi ya rais wake.
Mali ambayo ni jirani wa Burkina Faso, mwaka uliopita pia iliwakaribisha mamluki wa Wagner, ili kuwasaidia kwenye vita dhidi ya wanamgambo.