Rais wa Kenya William Ruto ameapa Jumatatu kuandaa mkutano wa ana kwa ana, kati ya majenerali wanaohasimiana nchini Sudan ili kumaliza mzozo unaolikumba taifa hilo baada ya makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano kushindwa kufanyika, ofisi ya rais wa Kenya imesema.
Mapigano yameendelea katika nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika tangu kati-kati ya mwezi Aprili, wakati mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza kikosi cha wanamgambo wa Rapid Support Forces waliposhambuliana.
Makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano yamefikiwa na kuvunjwa huku wapatanishi wa Marekani na Saudi Arabia wakionya Jumamosi kwamba huenda wakavunja juhudi za upatanishi ikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano ya saa 24 hayata-heshimiwa.
Pamoja na juhudi za Marekani na Saudi Arabia, Umoja wa Afrika umeisimamisha uanachama Sudan kufuatia mapinduzi ya mwaka 2021 yaliyoongozwa na Burhan na Daglo, na jumuiya ya kikanda ya Afrika Mashariki (IGAD) inashinikiza majadiliano yaliyosimamiwa na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir.
Forum