Rais wa Rwanda Paul Kagame ameongoza wananchi wake Ijumaa katika zoezi la kupiga kura ya maoni ili kubadili katiba nchini humo.
Wananchi nchini humo walijitokeza kwa wingi kuitikia mwito huo tangu alfajiri na kupanga foleni ya upigaji kura.
Kulikuwa na waangalizi wa ndani ya nchi hiyo ambao wameeleza kwamba kila kitu kimeenda vizuri kama walivyopanga.
Lakini wanadiplomasia kutoka maeneo mbali mbali wametoa wasi wasi wao na kutokuunga mkono hatua hiyo .
“Mataifa yote ya Umoja wa Ulaya yana msimamo sawa juu ya hili na tunaamini katika makabidhiano ya madaraka na sisi tunalitazama hili kupitia taswira ya kile kinachoonekana katika kanda hii ya Afrika ambapo viongozi wa mataifa wana badili katiba kwa ajili ya kusalia madarakani” alisema Michael Ryan mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini Rwanda.
Naye rais Kagame hakutaka kuongea na vyombo vya habari mpaka kura hiyo itakapokamilika na wala hajatoa msimamo wake juu ya kugombea muhula wa tatu.