Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC ameteuwa baraza jipya la mawaziri nchini humo zaidi ya mwaka mmoja baada ya kutoa ahadi ya kufanya hivyo. Rais aliita serikali hiyo kuwa ya mshikamano wa kitaifa ambapo inajumuisha pia mawaziri kutoka vyama vya upinzani.
Baraza jipya lina mawaziri 47 pamoja na Waziri Mkuu Matata Ponyo ambae anaendelea kushikilia wadhifa wake. Tofauti na serikali iliopita baraza hili la mawaziri limejaa viongozi wa vyama vya siasa.
Waziri Mkuu amepewa manaibu waziri wakuu watatu. Evariste Boshab katibu mkuu wa chama tawala PPRD ameteuliwa kuwa naibu waziri mkuu wa mambo ya ndani, huku Thomas Luhaka katibu mkuu wa chama cha upinzani cha MLC cha JP.Bemba alitajwa kuwa naibu waziri mkuu anayehusika na wizara ya posta , mawasiliano na teknolojia ya kisasa.
Wakati huo huo vyama vikuu vya upinzani nchini humo kama vile UDPS na UNC vilisusia kuingia kwenye serikali ya mseto. Chama cha UFC cha spika wa senet Leon Kengo wa Dondo kimepewa nafasi tatu serikalini. Kwa ujumla upinzani unamawaziri 7 hivi sasa.
Miongoni wa viongozi wa vyama vya siasa walioko kwenye baraza jipya la mawaziri ni pamoja na Bahati Lukwebo na Olivier Kamitatu. Ni mawaziri 10 pekee ambao wataendeleo kushikilia nyadhifa zao akiwemo waziri wa habari DRC, Lambert Mende, waziri wa mambo ya nje Raymond Tshibanda na Maker Mwangu waziri wa elimu ya msingi. Pia kuna wanawake saba wakiwa miongoni mwa mawaziri 47 wanaounda baraza jipya la mawaziri.
Ijapokuwa ni ahadi ya mwaka mmoja lakini wachambuzi wa masuala ya siasa wanaeleza kwamba baraza hili linalenga kuwatuliza wapinzani wanaoelekeza kidole kwa chama tawala kubadili katiba.
Na vyama vikuu vya upinzani vinakosowa vikali baraza hilo vikieleza kwamba hakuna mabadiliko yaliyofanyikia. Mshauri wa kisiasa wa chama cha UPDS, Valentine Mubake anasema wajumbe wa upinzani walojiunga na serikali hiyo hawakupata ridhaa ya vyama vyao.
Serikali hii mpya inajumuisha mawaziri ambao wameunga mkono mageuzi ya katiba na wale wanaopinga mageuzi hayo.
Miongoni mwa wale wanaounga mkono mageuzi hayo ya katiba ni pamoja na katibu mkuu wa chama tawala cha PPRD, Everist Boshab, huku Olivier Kamitatu kiongozi wa chama cha ARC na ambae ameteuliwa kuwa waziri wa mipango ya serikali yeye ni miongoni mwa wanaopinga pendekezo hilo la kurekebisha katiba ya nchi hiyo. Tangu kuzuka kwa mjadala huo Rais Kabila bado hajaelezea msimamo wake.
Maoni ya watu yanatofautiana baada ya kuteuliwa kwa baraza jipya la mawaziri ambapo wakaazi wa Kinshasa wanasubiri kuona utendaji kazi wake, huku chama cha MLC kikiwa tayari kimeshagawanyika. Baadhi ya wafuasi wa chama hicho wanasema hatua ya katibu mkuu wa chama chao kuingia serikalini ni tofauti na msimamo wa chama. Hivyo viongozi hao wamejitenga na chama.