Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Januari 20, 2025 Local time: 17:04

Obama asitisha kwa muda uteuzi wa Allen


Jenerali John Allen
Jenerali John Allen
Rais wa Marekani Barack Obama ameamuwa kutomteuwa kwa wakati huu Jenerali John Allen kama kamanda mkuu wa NATO, akisubiri matokeo ya uchunguzi wa shutuma za mawasiliano yanayokwenda kinyume na maadili yaliyomuhusisha kamanda huyo wa Marekani nchini Afghanistan na mwanamke mmoja aliyehusishwa kwenye kashfa ambayo ilipelekea kujiuzulu kwa mkuu wa idara ya ujasusi ya Marekani CIA, Jenerali David Petraeus.

Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa, Tommy Vietor anasema Rais Obama alichelewesha kutangaza uteuzi huo uliowasilishwa na waziri wa ulinzi Leon Panetta.

Bwana Obama alimteuwa Jenerali Allen kuchukua nafasi kama Mkuu wa Majeshi ya Ushirika ya Ulaya, mwezi mmoja kabla ya Petraeus kujiuzulu Ijumaa iliyopita kutokana na kashfa ya mapenzi nje ya ndoa.

Shutuma dhidi ya Jenerali Allen zinahusisha mawasiliano ya barua pepe na Jill Kelley ambaye anaelezewa kama rafiki wa familia ya Petraeus.

Malalamiko yake kwa idara ya serikali ya upelelezi wa jinai-FBI kuhusu vitisho vya barua pepe kutoka kwa mwanamke mmoja aitwaye Paula Broadwell ambaye Petraeus alikuwa na mahusiano naye kimapenzi, na ndiye aliyeandika kitabu juu ya maisha yake ndiyo ilifichua kashfa na kumpelekea mkuu huyo wa CIA kujiuzulu.

Afisa mmoja mwandamizi wa wizara ya ulinzi anasema FBI inachunguza kati ya kurasa 20,000 hadi 30,000 za mawasiliano zinazomhusisha Jenerali Allen na Kelley, barua pepe ambazo zilitumwa kati ya mwaka 2010 na 2012.

Msemaji wa Pentagon, George Little alisema FBI iliwasilisha tatizo hilo linalomhusisha Jenerali Allen kwa wizara ya ulinzi siku ya Jumapili na Panetta alitoa maelekezo kwa inspekta mkuu wa Pentagon kulifanyia uchunguzi suala hili.

Jenerali Allen anakanusha kufanya kosa lolote na ataendelea na nafasi yake ya kamanda huko Afghanistan katika kipindi cha uchunguzi.
XS
SM
MD
LG