Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen ameeleza kuwa hana matumaini mazuri kutokana na mpango wa kusitisha mapigano nchini Ukraine ulopendekezwa na Rais wa Russia Vladmir vPutin, wakati viongozi wa mataifa makuu ya dunia wanakutana mjini Wales kwa ajili ya mkutano muhimu wa viongozi wa NATO.
Bw. Rassmusen alisema Alhamisi kwamba, NATO inakaribisha juhudi zote za kupata suluhisho la Amani kuhusiana na mzozo wa Ukraine. Lakini akaongeza kuwa, cha muhimu ni kuona jinsi hali itakavyoenedelea katika eneo la mapigano, akisisitiza kwamba Russia bado “inaishambulia” Ukraine.
Mkutano huo wa siku mbili wa viongozi wa NATO unaofanyika nje kidogo ya mji wa Newport, huko Wales unatarajiwa kujadili kuhusu kuunda kikosi cha jeshi cha dharura kitakachoweza kuinglia kati kwa haraka katika maeneo yenye mizozo huko Ulaya Mashariki.
Russia ambayo daima imepinga kuwepo kwa wanajeshi wowote wa NATO karibu na mipaka yake, tayari imeshalaani wazo hilo la kikosi cha dharura . Mapema wiki hii Russia ilieleza kuwa itatathmini mikakati yake ya kijeshi Ulaya Mashariki kama NATO itaidhinisha kuundwa kwa kikosi hicho.
NATO inakadiria karibu wanajeshi elfu moja wa Russia wapo Ukraine. Moscow imekanusha mara kwa mara kuwepo kwa wanajeshi wake katika ardhi ya Ukraine.
Viongozi katika mkutano wa NATO wanatarajiwa pia kuzungumzia mikakati ya kukabiliana na vitisho vinavyotokana na kundi la wanamgambo wa kislamu la Islamic State linaloshikilia sehemu kubwa ya kaskazini ya Iran na mashariki ya Syria.