Rais wa Marekani Joe Biden amesema Jumanne kwamba mkutano wa kilele wa NATO wa mwaka huu unawakilisha wakati wa kihistoria, wakati jumuiya hiyo ya usalama ikijiandaa kupanuka huku ikishughulikia masuala yanayozunguka vita vya Ukraine.
“Huu ni wakati wa kihistoria,” Biden alimwambia Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg. “Kuiongeza Finland na Sweden kwenye uanachama wa NATO ni muhimu. Uongozi wako una tija sana. Na tunakubaliana juu ya lugha unayopendekeza, kuhusiana na mustakbali wa Ukraine kuweza kujiunga na NATO,” aliongeza.
Stoltenberg amesema Jumanne kwamba ana imani kubwa bunge la Uturuki litamkubali mwanachama mpya, Sweden. Wakati huo huo, Rais wa Ukraine aliendelea kushinikiza taifa lake kuingia katika muungano huo wa usalama, hatua ambayo wanachama wa NATO wanaonekana kuwa hawawezi kufanya katika mkutano huo wa kilele unaofanyika katika mji mkuu wa Lithuania.
“NATO itaipa Ukraine usalama,” aliandika rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy. “Ukraine itafanya muungano huo kuwa imara zaidi,” aliongeza. Washirika walikuwa wakijadili maneno ya maandishi ya mwisho ya pamoja, lakini kuna makubaliano kwamba Ukraine kujiunga na NATO wakati uvamizi wa Russia unaendelea sio jambo muafaka.
Forum