Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden na Seneta anayewakilisha jimbo la California, Kamala Harris, wanatarajiwa kukubali rasmi uteuzi wa chama chao, kama Mgombea urais na mgombea mwenza mtawalia.
Pamoja na wao kukubali uteuzi huo, hafla mbalimbali zimepanwa kufanyika katika siku hizo nne, na viongozi wa ngazi ya juu kwenye chama hicho, wakiwa ni pamoja na rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, kutoa hotuba zao.
Kwa mujibu wa ratiba ya mikutano hiyo, Obama atazungumza siku ya Jumatano.
Wengine watakaotoa hotuba ni waliokuwa wagombea urais Bernie Sanders, Amy Klobuchar, Elizabeth Warren, Cory Booker, Pete Buttigieg na John Kasich (Mrepublikan).
Wengine ni mke wa aliyekuwa rais, Michelle Obama, Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton na mkewe Hillary Clinton.
Wanasiasa John Kerry, Alexandria Ocasio-Cortez pia watahutubia wafuasi wao.
Chama hicho kimesema nyingi za hotuba zitafanyika kwa njia ya mtandao.
Ingawa kwa kawaida mikutano mikuu ya vyama huvutia maelfu ya watu, mwaka huu hali ni tofauti na wafuasi wengi wa chama hicho wanatarajiwa kutazama au kufuatilia yatakayojiri kupitia vyombo vya habari.
"Mkutano wa mwaka huu utakuwa na utofauti mkubwa mno na mikutano ya miaka iliyopita kwa sababu unafanyika katika mazingira ya janga la Corona, hali mabayo haijawahi kushuhudiwa tena katika historia ya Marekani," alisema Dkt Patrick Nighula, Mhadhiri wa chuo kikuu cha South Carolina, akizungumza na Sauti ya Amerika kwa njia ya simu Jumapili usiku.
Jumapili, White House ilikubali kwamba Seneta Kamala Harris anaweza kuwa makamu rais, na kumaliza tetesi zilizokuwa zikirudiwa na Rais Donald Trump kwamba mwanasiasa huyo alikuwa hastahili kuhudumu wadhifa huo.
Harris alizaliwa nchini Marekani na wazazi wahamiaji na RaisTrump amekuwa akikosolewa kwa kutochukua msimamo wa wazi kuhusu tetesi hizo.
Mkutano mkuu wa chama cha Republikan utaanza Jumatatu tarehe 24 Agosti na kwendelea hadi Alhamisi tarehe 28 ambapo Rais Donald Trump pamoja na makamu wake, Mike Pence, wanatarajiwa kukubali uteuzi wa chama chao wa kugombea urais kwa muhula wa pili.