Alikuwa ni mchezaji hatari wa Misri ambaye anaichezea pia timu ya Aston Villa, Mahmoud Ahmed Ibrahim Hassan au maarufu Trézéguet aliyepachika bao la pili na la ushindi katika dakika ya 100 katika muda wa nyongeza na kuihakikishia Misri nafasi ya kutinga katika nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010.
Hata hivyo ilikuwa ni Morocco iliyoanza vyema mchezo huo wakati Sofiane Boufal alipofunga bao la kwanza kwa njia ya penati katika mchezo huo kwenye dakika ya 6 ambapo uamuzi huo ulichukuliwa kufuatia ukaguzi wa VAR.
Katika kipindi pili Mo Salah aliipatia timu yake bao la kusawazisha katika dakika ya 53 na pia mchezaji huyo wa Liverpool alitoa asisti iliyopelekea Trezeguet kupachika bao.
Mchezo huo ulikuwa na mvutano mkali kwa nchi hizi mbili zinazofahamiana katika soka ambapo jumla ya kadi 6 za njano zilitolewa ambapo katika tukio moja karibu wachezaji hao wapigane baada ya Mohamed Abdelmonem kumsukuma mshambuliaji wa Morocco Selim Amallah ambapo mpira ulisimama kwa dakika chache ukihusisha mpaka benchi la ufundi kuingia uwanjani na refa na wasaidizi wake kufanya kazi ya ziada kuwazuia wachezaji hao waliokuwa wamejawa na jazba.
Refa na wasaidizi wake walidhibiti tafrani hiyo na kutoa kadi za njano kwa Selim Amala wa Morocco na beki Mohamed Abdelmonem wa Misri.
Sasa Mafarao wa Misri watamenyana na wenyeji Cameroon katika nusu fainali, huku wakisaka taji lao la kwanza la AFCON tangu mwaka 2010.