Mfalme wa Uingereza Charles III anarejea London leo Ijumaa kutoka Balmoral Castle huko Scotland ambako mama yake, Malkia Elizabeth, alifariki siku ya Alhamisi.
Charles, ambaye ana umri wa miaka 73 na mfalme mwenye umri mkubwa zaidi kutwaa kiti hicho cha enzi, amepangiwa kutoa hotuba kwa njia ya televisheni kwa taifa katika maombolezo ya Ijumaa, ikiwa hotuba yake ya kwanza kama mkuu wa nchi.
Mfalme pia anatarajiwa leo Ijumaa kufanya mkutano wake wa kwanza na Waziri Mkuu Liz Truss kwenye kasri ya Buckingham. Malkia Elizabeth alimteua Truss katika wadhifa wake mpya kama waziri mkuu siku ya Jumanne, siku mbili tu kabla ya kifo chake.
Bunge linafanya kikao maalum leo mchana kutoa heshima kwa Malkia. Truss na wahudumu wengine pia wanatazamiwa kuhudhuria ibada ya kumbukumbu ya Malkia hivi leo katika Kanisa Kuu la Mt. Paul.