Mapema mwezi huu, mahakama ya kazi ya Kenya ilitoa uamuzi kuwa Meta inaweza kushtakiwa nchini humo baada ya aliyekuwa msimamizi wa maudhui kufungua mashtaka akidai wafanyakazi walifanyishwa kazi katika mazingira magumu.
Kwenye rufaa hiyo ambayo shirika la habari la Reuters liliweza kuiona Jumanne, kampuni hiyo ya Marekani ilihoji uamuzi wa mahakama kwamba mahakama za Kenya zina mamlaka ya kisheria juu ya kampuni hiyo ya Meta.
Meta iliajiri wafanyakazi kutoka nje kudhibiti maudhui yake kupitia Sama, kampuni yenye makao makuu Marekani na kuendesha shughuli zake nchini Kenya. Mwezi uliopita Sama ilisema haitatoa tena huduma za udhibiti wa maudhui kwenye kampuni ya Meta.
Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa msimamizi wa maudhui Daniel Motaung kwa niaba ya kundi la waliokuwa wafanyakazi wa Sama.