Waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi, ameahidi kufanya mabadiliko kamili ya serikali hapo October, ambayo yatakua ni pamoja na mabadiliko ya mfumo wa afisi za ubalozi wa nchi yake katika nchi za nje.
Kiongozi huyo wa Ethiopia alikutana na waandishi habari Jumanne na kuwaeleza kwamba kile alichokieleza kuwa ni kipindi kigumu cha uhusiano na Marekani kinaelekea kumalizika.
Amesema balozi wake mpya huko Washington, atatangazwa hivi karibuni wakati wa kutangaza mabadiliko makubwa ya serikali.
"Nadhani kile kipindi kigumu cha kati ya miezi 6 hadi 7 ilopita, sasa kwa kiwango kikubwa kimeshapita. Kuna masuala ambayo maafisa huko Marekani wanahisi kwa dhati yanatofatuiana kabisa na sisi, na kuna masuala ambayo sisi tunahisi kwa dhati yanatofautiana nao. Tutakubaliana, kutokukubaliana, na tunakubali kufanya kazi pamoja kwenye masuala ya maslahi ya pamoja,"alisema Zenawi.
Uhusiano kati ya nchi hizi mbili ulifikia kiwango cha chini kabisa hapo mwezi Mei , wakati wa kufanyika kwa uchaguzi wa bunge wa Ethopia. Hakuna makundi ya wafatiliaji kutoka Marekani waloruhusiwa kwenda nchini humo, na wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani walipigwa marufuku kutembelea vituo vya upigaji kura au kusafiri nje ya mji mkuu Addis Ababa siku ya uchaguzi.
Ikulu ya Marekani ilijibu kwa kutowa taarifa yenye maneno makali. Ilisema uchaguzi haukufikia kiwango cha kimataifa, na ikaikosoa serikali ya Ethiopia kwa kushindwa kubuni mazingira yanofaa ili kuwepo na uchaguzi wa haki na wa huru.