Rais wa Marekani, Barack Obama ametoa amri kwa bendera za Marekani kupepea nusu mlingoti kwa heshima ya kuwakumbuka waathirika waliouwawa katika shambulizi baya la watu wengi kuliko yote katika historia ya Marekani.
Mtu mmoja mwenye silaha aliuwa watu wapatao 50 na kujeruhi 53 wengine ndani ya klabu ya usiku ambayo hutumiwa zaidi na mashoga huko Orlando Florida Jumapili alfajiri.
Obama alitangaza kuwa kicho ni kitendo cha kigaidi na kusema FBI wanaongoza uchunguzi. Amesema juhudi zote zinafanyika kujua nini kilimchochea muuaji huyo kufanya hivyo au kama alikuwa na ushirikiano wowote na makundi ya kigaidi.
Rais aliyekuwa amesikitishwa sana alilihutubia taifa lililopigwa na butwaa kutokea White House akisema ni rahisi kwa mtu kupata silaha kuwapiga watu mashuleni, makanisani, kwenye majumba ya sinema na klabu za usiku. Mwanasheria mkuu Loretta Lynch na waziri wa usalama wa ndani Jeh Johnson wote waliakhirisha safari zao kwenda Beijing kwa mazungumzo juu ya usalama wa mitandao na maafisa wa China.