Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 08, 2025 Local time: 18:42

Matatizo yanayowakumba wakimbizi pembe ya Afrika


Wakimbizi wa kisomali wanasubiri kwa mrondo kupokea chakula katika kituo cha WFP ndani ya kambi ya Dadaab, Kenya, Julai 15, 2011
Wakimbizi wa kisomali wanasubiri kwa mrondo kupokea chakula katika kituo cha WFP ndani ya kambi ya Dadaab, Kenya, Julai 15, 2011

Idadi ya wakimbizi ikiongezeka kutoka Somalia kuingia Kenya, hali inazidi kuwa ngumu kwa wakimbizi walofurika tayari katikakambi kuu ya wakimbizi Afrika ya Dadaab

Inakadiriwa wasomali 1,500 wanavuka mpaka na kuingia Kenya kila siku wakisaka ahueni kutoka na madhila yanayowasibu nyumbani somalia. Neno hifadhi huko Dadaab limesambaa kote nchini, na kuchochea wengi kujiingiza katika safari ndefu yenye hatari, mara nyingi wakitembea kwa miguu kwa matumaini ya kupata maisha bora.

Wengi hawamalizi safari yao kwa usalama, ambayo huwachukua zaidi ya mwezi mmoja. Lakini wale ambao wananusurika mara nyingi wanapata ahueni kwa kupewa chakula cha kutosha, maji na makazi ambayo hutolewa na mashirika ya misaada yanayofanya shughuli zao katika kambi hizo.

Kwa baadhi yao, hata hivyo, ahueni haiji haraka hivyo. Mmiminiko mkubwa wa wakimbizi katika miezi ya karibuni umefurika katika kambi, na kuchota rasimali za mashirika hayo yanayojaribu kusaidia. Wakimbizi wanapowasili mara ya kwanza huko Dadaab, wanapatiwa mgao wa awali wa chakula ambao unatarajiwa kudumu kwa mpaka pale watakapoandikishwa rasmi na kupatiwa kadi za mgao.

Lakini wakimbizi wengi wanawasili kila siku, kujiandikisha kunachukua muda mrefu, na kuwaacha watu wakijisaidia wenyewe wakati wakisubiri kuandikishwa rasmi kama wakimbizi.

Nurta Heirat aliondoka Baidoa na watoto wake wawili mwezi june akikimbia ukandamizaji wa kundi la waasi wa kiislamu la al-Shabab. Familia yale ilitembea kwa siku 20 hadi kufika dadaab, ambako walipatiwa mgao wa awali. Lakini hadi hivi sasa baada ya zaidi ya wiki mbili katika kambi, chakula chao kimewaishia.

Nurta anarejea kila siku kwenye kituo cha uandikishaji cha UNHCR katika kambi ya Dagahaley kwa matumaini ya kupatiwa kadi ya mgao lakini hadi sasa bado hajafanikiwa.

Heirat na watoto wake bado wanalala kwenye hema. Ilikuwa ni kwa bahati tu aliweza kuonana na mpwa wake, Abdirashid Haji kwenye kambi hiyo, ambaye alimpatia msaada kiasi wiki iliyopita.

Hadithi ya nurta kwa bahati ni ya kawaida. Shinikizo kubwa la kibinadamu ambalo limesababishwa na mmiminiko wa karibuni wa wasomali umefanya hali ya mgao kuwa katika kiwango cha kutsiha, kitu ambacho mashirika ya misaada yanajaribu kuzungumzia tatizo hili.Rose Ogola ni msemaji wa shirika la mpango wa chakula huko Dadaab.

“Awali tulipoanza kugawa chakula hapa katika vituo vya mapokezi, tulianza kwa kutoa mgao wa siku 15 tukitumaini kuwa watu hawa katika muda huo wa siku 15, watakuwa wameandikishwa na tunaweza kuwaweka katika daftari. Hata hivyo kwasababu ya mmiminiko mkubwa, tumebaini utaratibu huu haufanyi kazi. Kwahiyo tangu july 15 tumebadili mkakati na badala ya kutoa mgao wa siku 15 tunatoa mgao wa siku 21.”

Huku wakimbizi wakiendelea kuingia dadaab, pengine mgao huo wa siku 21 pia hautasaidia. Baadhi ya wale wanaowasili wameripotiwa kusubiri mpaka siku 40 kuweza kupata kadi za mgao, na kuwaacha wakiwa hawana chakula cha kuwasaidia kwa muda.

Changamoto pia zinajitokeza mara wakimbizi wanapopewa hifadhi katika kambi.

Yusuf Ali na Fatumah Muhamud walifika kutoka Somalia mwaka 2008, walikimbia mapigano katika eneo leo. Awali walipewa hifadhi katika kambi ya Dagahaley na walipata matatizo kidogo mpaka pale mtoto wao wa kike mwenye umri wa miaka 15 alipobakwa. Wazazi hao waliripoti uhalifu huo kwa UNHCR, ambao haraka walimkamata mtu aliyehusika na kutiwa jela.

Lakini jamaa wa mshambuliaji huyo walianza kusababisha matatizo kwa ali na Muhamud wakiwataka waondoke Dagahaley, na hata walijaribu kumteka mtoto wao wa kike. Hivi karibuni, ali na Muhamud waliondoka na familia yao huko Dagahaley kwa khofu ya kulipiziwa kisasi na familia ya mshambuliaji. Tangu wakati hauo wamekuwa wakilala karibu na kituo cha uandikishaji huko Dagahaley kwa matumaini ya kuhamishiwa kambi nyingine au eneo jingine la kenya.

Ingawaje wakimbizi kote katika kambi huko Dadaab wanapata hifadhi kutokana na matatizo mbali mbali yaliyowakabili nchini Somalia, wengi wanasema magumu ya safari na changamoto za kujenga tena maisha yao zimekuwa ni za gharama kubwa. Janeto Ndoti Ndila anafanyaka kazi katika shirika la Care International kama mshauri huko Dagahaley.

Ndila anasema baadhi ya wale aliozungumza nao kwa kweli wanamasikitiko kwa uamuzi wa kuondoka.

“Hasa wakati mwingine wakiwa njiani wanapoteza mali zao. Hiyo ni moja ya mabo ambayo yanawafanya wasema bora nisingekuja hapa. Tumepoteza mali zetu, nimepoteza ng’ombe wangu, nimepoteza dhahabu zangu. Sina chochote.”

Mashirika ya misaada ikiwa ni pamoja na Care, shirika la mpango wa Chakula Duniani na UNHCR wanajitahidi kukidhi mahitaji ya idadi ya watu wanaofurika huko Dadaab, lakini rasimali zilizopo hazitoshi hata kidogo. Takriban nusu ya makadirio ya dola bilioni mbili zinazohitajika kuzungumzia mzozo wa afrika mashariki ndiyo zimetolewa hadi sasa.

Uhaba wa vifaa muhimu kama vile mahema, inasababisha wakimbizi wapewe mabati ya plastiki kujenga makao yao kwenye viunga vya kambi. Huku rasimali za kibinadamu zikiwa zinazidi kupungua, wakimbizi wengi inawalazimu wasubiri kupata misaada ambayo wameisafiria mamia ya maili ili kuipata.

XS
SM
MD
LG