Serikali ya Mali imeweka saini mpango wa awali wa amani na baadhi ya makundi ya waasi wa kaskazini mwa nchi.
Pamoja na hayo muungano mkuu wa waasi wa Tuareg umehitaji muda zaidi wa kutafakari kabla ya kukubali makubaliano hayo.
Wanachama wa muungano wa waasi wa Tuareg ambao unajumuisha kundi la kitaifa la ukombozi wa Azawad, lilihudhuria uwekwaji wa saini katika mji mkuu wa Aljeria, Algies.
Wawakilishi wa muungano huo walisema wataendelea na mazungumzo na kuongeza kwamba walihitaji muda zaidi.
Mpango huo unaosimamiwa na umoja wa mataifa ni mahsusi kwa kumaliza hali ya ukosefu wa usalama na kutoelewana huko kaskazini mwa Mali.
Kundi la waasi wa Tuareg linataka kupewa mamlaka ya ndani ya eneo hilo.
Mali imekuwa katika hali ya machafuko tokea wapiganaji wa Tuareg walipoanzisha ghasia mwanzoni mwa mwaka 2012 tukio lililochochea mapinduzi mjini Bamako.