Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 11:54

Mali yasema EU haitaondoa uwakilishi wake


Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop

Serikali ya Mali imetoa uhakikisho kuwa Umoja wa Ulaya (EU) hautaondoa uwakilishi wake nchini Mali lakini kuna mipango kuwa itafanya baadhi ya mabadiliko jinsi utakavyojishirikisha nchini humo.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop katika mahojiano maalum na Sauti ya Amerika, aliongeza kuwa wamewasiliana na EU kuelezea kuwa mamlaka iko wazi katika kuendeleza ushirikiano wao, akituamini kuwa EU itaamua kuendelea na mazungumzo ambayo yanafanyika. “Tunasubiri kupata ufafanuzi zaidi katika mabadiliko ya operesheni za EU nchini mali,” Diop amesema.

Kuhusu ushirikiano na Russia, Waziri Diop amesema kuwa nchi yake imefanya mchakato wa kimkakati kuongeza wigo na washirika wake ikiwemo kufanya kazi na Russia, na kuongezea kuwa ushirikiano huo unazaa matunda na matokeo yanatia moyo.

“Mali itaendelea kuwa nchi yenye kukaribisha washirika wake wote, Magharibi na Mashariki ambao watapenda kuja kufanya kazi kwa kufuata dira yetu na vipaumbele ambavyo tumeviweka katika nchi yetu,” amesema Diop.

Jeshi la Ufaransa la Barkhane Force likilinda doria mitaa ya Timbuktu, magharibi ya Mali Disemba 5, 2021. (Photo by Kay Nietfeld / POOL / AFP)
Jeshi la Ufaransa la Barkhane Force likilinda doria mitaa ya Timbuktu, magharibi ya Mali Disemba 5, 2021. (Photo by Kay Nietfeld / POOL / AFP)

Hata hivyo Waziri Diop amevitahadharisha vyombo vya habari iwe vya ndani au nje kuwa waangalifu na vyanzo vya taarifa zao, akisema baadhi ya ripoti ni za uzushi ambazo zinahusu tuhuma za mauaji yanayofanywa na jeshi na zinaweza kupandikiza mbegu za chuki.

Ametoa mfano wa taarifa ambazo kuna baadhi ya mashuhuda walitoa siri huko Jamhuri ya Afrika ya Kati kwamba walilipwa kutoa ushahidi wa uongo, “tunafahamu kuna ushawishi wa kuvuruga mchakato wa kipindi cha mpito na kulikatisha tamaa jeshi letu,” aliongezea.

Kuhusu ripoti ambazo zinamfikia kutoka jamii za Moura na Fulani, amesema hakuna mauaji ambayo yamefanyika na jeshi la nchi lina weledi mkubwa na limekuwa likifuata sheria na kuheshimu haki za binadamu.

Diop alisema wanazo taarifa maalum za kijasusi zinazoonyesha kuwa magaidi ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakijificha huko Moura wanajikusanya na pia wamekuwa wakitenda uhalifu dhidi ya raia, ingawaje wananchi hawajazungumzia kile ambacho wanafanyiwa na magaidi hao, ikiwemo ukatili wa kijinsia, mauaji ya watu, kuwatoza ushuru kwa nguvu na kuweka vizuizi vya kutoondoka maeneo hayo, akihoji je hayo siyo masuala ya kibinadamu.

Waziri amesema kuwa uchaguzi ni muhimu, lakini kuna vitu vya kuzingatiwa kabla ya kufikia maamuzi ya kuitisha uchaguzi mkuu. Amesema bado kuna tofauti kati ya muda ambao umependekezwa na serikali, ambao ni miezi 24 ya mashauriano.

“Tumeridhia mambo muhimu, hasa tukizingatia muda ambao ni muafaka, na kuangalia baadhi ya malengo ambayo serikali inataka kufanikisha hasa katika kuweka hali nzuri ya ulinzi katika nchi, na kushughulikia masuala muhimu ya kitaasisi na mageuzi ya kisiasa ili kuhakikisha kwamba mchakato wa demokrasia nchini Mali hauwezi kubadilishwa,” amongezea.

Marais wa ECOWAS na wawakilishi wengine wakiwa katika picha ya pamoja mjini Accra, Ghana, Ijumaa Machi 25, 2022. Baada ya kikao kilichowawekea Mali vikwazo kufuatia mapinduzi ya kijeshi nchini Mali. AP Photo/Misper Apawu)
Marais wa ECOWAS na wawakilishi wengine wakiwa katika picha ya pamoja mjini Accra, Ghana, Ijumaa Machi 25, 2022. Baada ya kikao kilichowawekea Mali vikwazo kufuatia mapinduzi ya kijeshi nchini Mali. AP Photo/Misper Apawu)

Waziri amesema serikali inafahamu kuwa umoja wa kikanda ECOWAS umetoa pendekezo la kuitisha uchaguzi katika muda wa miezi 12 mpaka 16, na hilo liko mezani, lakini bado halijazingatiwa, kwa sababu wajibu hivi sasa uko kwa serikali ya Mali na wananchi wa Mali kufahamu kwanza hali halisi ndani ya nchi. Kuna mengi ambayo tunakabiliana nayo, ikiwemo suala la usalama, mzozo wa uongozi, matatizo ya kiuchumi na kijamii.

Kilicho muhimu kwa wakati huu ni kuhakikisha kiwango cha usalama kimeimarishwa na miundo mbinu iko katika mfumo unaokubalika ili kurahisisha usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi kwenda maeneo tofauti ya nchi. Bado tuko katika mazungumzo na taasisi ya kikanda, lakini kinachozingatiwa zaidi, “ni muda gani unahitajika kukamilisha marekebisho yote yanayohitajika na kufanya maandalizi ya uchaguzi na kumaliza kipindi cha mpito na kuirejesha nchi katika hali ya utulivu wa kudumu na utawala.”

XS
SM
MD
LG