Majadiliano ya jopo la mahakama yalianza Jumatano katika kesi ya Donald Trump ya malipo ya kumnyamazisha mwanamke mcheza filamu za ngono, hivyo kuweka matokeo ya kesi hii ya kihistoria mikononi mwa wakazi kumi na wawili wa New York ambao wameapa kuwa waaminifu na wasio na upendeleo katika kazi yao isiyo ya kawaida.
Jopo hilo la wanaume saba na wanawake watano lilipelekwa katika chumba cha faragha muda mfupi kabla ya saa 5:30 asubuhi Jumatano kuanza kujadili hukumu katika kesi ya kwanza ya jinai ya rais wa zamani wa Marekani. Majadiliano ya jopo hilo yatakuwa ya siri, ingawa wanaweza kutuma maelezo kwa jaji kuomba kusikiliza tena ushahidi au kuona ushahidi. Hiyo pia ndiyo njia watakayotumia kuiarifu mahakama juu ya hukumu, au ikiwa hawataweza kufikia maamuzi ya pamoja.
"Siyo jukumu langu kuhukumu ushahidi hapa. Ni jukumu lenu," Jaji Juan M. Merchan aliwaambia wajumbe hao wa jopo la mahakama.
Trump alionyesha hisia za kukata tamaa baada ya kuondoka katika chumba cha mahakama baada ya kupata maelekezo ya jaji kwa saa moja, akirudia madai yake ya "kesi isiyo ya haki sana" na kusema: "hata Mama Teresa asingeweza kushinda mashtaka haya. Mashtaka haya yamepangwa."
Trump na mawakili wake, pamoja na waendesha mashtaka, waliagizwa kubaki ndani ya jengo la mahakama wakati wa majadiliano. Alionekana akirudi nyuma kwenye kiti chake na kufumba macho wakati Jaji Merchan akitoa maelekezo kwa jopo.
Trump ameshtakiwa kwa makosa 34 ya kughushi kumbukumbu za biashara katika kampuni yake kuhusiana na mpango unaodaiwa wa kuficha taarifa za aibu kuhusu yeye wakati wa kampeni yake ya uchaguzi wa rais wa Republican mwaka 2016.
Shtaka hilo, ambalo ni kosa la jinai, linatokana na malipo ya fidia yaliyolipwa kwa wakili wa Trump wa wakati huo, Michael Cohen, baada ya kutoa malipo ya kimya ya dola 130,000 kwa muigizaji wa filamu za ngono, Stormy Daniels, ili kumnyamazisha kuhusu madai ya kwamba wawili hao walifanya ngono mwaka 2006. Trump anadaiwa kutoa taarifa za uongo za malipo ya Cohen kama gharama za kisheria ili kuficha kwamba zilikuwa na uhusiano na malipo ya kumnyamazisha mwanamke huyo.
Trump amekana mashtaka na anadai malipo ya Cohen yalikuwa kwa huduma halali za kisheria. Pia amekana tukio la kingono nje ya ndoa na Daniels.
Ili kumhukumu Trump, jopo la wajumbe wa mahakama litahitaji kukubaliana kwa pamoja kwamba ana hatia ya kughushi rekodi za kampuni yake, au alisababisha mtu mwingine kufanya hivyo, na kwamba alifanya hivyo kwa nia ya kufanya au kuficha uhalifu mwingine.
Uhalifu ambao waendesha mashtaka wanasema Trump alifanya ni uvunjaji wa sheria za uchaguzi za New York zinazofanya kuwa haramu kwa washirika wawili au zaidi "kukuza au kuzuia uchaguzi wa mtu yeyote katika ofisi ya umma kwa njia zisizo halali."
Mwendesha mashtaka Joshua Steinglass aligusia dhana ya uwajibikaji wa kijinai katika hoja yake ya mwisho Jumanne, akiwaambia wajumbe wa mahakama: "Hakuna anayeweza kusema mshtakiwa alikaa nyuma ya kompyuta na kuandika vocha za uongo au kupiga mihuri ankara za uongo au kuchapisha hundi za uongo."
"Lakini aliweka mnyororo wa matukio uliopelekea kuundwa kwa rekodi za biashara za kughushi," Steinglass alisema.
Hukumu yoyote lazima iwe ya pamoja. Wakati wa majadiliano, wajumbe sita mbadala ambao pia waliketi kila dakika ya kesi watakuwa wakiwekwa kwenye jengo la mahakama katika chumba tofauti iwapo watahitajika kuchukua nafasi ya jaji ambaye anaumwa au hana uwezo. Ikitokea hivyo, majadiliano yataanza upya mara baada ya wajumbe mbadala kuwa mahali pake.
Forum