Maafisa wa afya wa Misri wamesema wamegundua kesi za kwanza za ugonjwa corona aina ya Omicron nchini humo unaombukiza sana.
Watu watatu waligundulika wana maambukizi hayo kati ya wasafiri 26 waliopimwa na kukutwa na virusi hivyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo, Wizara ya Afya ilisema katika taarifa yake Ijumaa. Haikusema watatu hao walitokea wapi.
Chombo cha habari cha ndani cha Masrawy kiliripoti kuwa watatu hao walikuwa miongoni mwa wasafiri kutoka Afrika Kusini.
Wizara hiyo ilisema watu wawili kati ya walioambukizwa hawakuonyesha dalili zozote, huku wa tatu akiwa na dalili kidogo. Watatu hao wametengwa katika hospitali ya Cairo, ilisema.
Maafisa nchini humo siku ya Ijumaa waliripoti zaidi ya kesi mpya 900 zilizothibitishwa za corona na vifo 43 katika saa 24 yaliyopita.
Misri imeripoti jumla ya kesi 373,500, pamoja na vifo 21,277, tangu janga hilo kuanza.