Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 28, 2024 Local time: 14:51

Hali ya kutoaminiana ni tishio kubwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, asema Kenyatta


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akihutubia mkutano wa Atlantic Council mjini Washington DC kwa njia ya Video.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akihutubia mkutano wa Atlantic Council mjini Washington DC kwa njia ya Video.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema Alhamisi kwamba bado anaunga mkono juhudi za kuimarisha jumuiya ya Afrika Mashariki licha ya changamoto zilizopo na kukiri kuwa moja ya vizingiti vikubwa katika mchakato huo “ni hali ya kutoaminiana.”

Kenyatta aliyasema hayo wakati ambapo nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki zimekuwa zikikabiliana na changamoto mpya zinazotishia baadhi ya hatua zilizopigwa katika kuimarisha ushirikiano huo wa kieneo.

Changamoto za hivi karibuni kabisa zikisababishwa na janga la Korona, lililopelekea baadhi ya nchi kufunga mipaka katika juhudi za kukabiliana na maambukizi, hali ambayo imeleta misuguano ya hapa na pale ya kidiplomasia.

Kenyatta alikuwa akizungumza kwa njia ya video wakati wa mkutano ulioitishwa na kituo cha Afrika cha Baraza la Atlantic, chenye makao yake makuu mjini Washington DC, Marekani.

Sikiliza hapa:

please wait

No media source currently available

0:00 0:03:44 0:00

Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa washiriki wa mkutano huo, ambao kimsingi ulikuwa unajadili mahusiano a kibiashara kati ya Kenya na Marekani na mstakabali wa makubaliano yaliyotiwa Saini mapema mwaka huu kati yake na Rais Donald Trump, Kenyatta alisema mchakato wa kuimarisha jumuiya ya Afrika Mashariki umekabiliwa na changamoto chungu nzima.

“Tunakabiliwa pia na changamoto kubwa kutokana na sababu mbalimbali. Na pia kuna hali ya kutoaminina kati ya mambo mengine. Hii ndiyo imani niliyo nayo.. kwamba ni lazima tukabiliane na changamoto hizi, na njia ya kukabiliana nazo ni kuja pamoja na kushirikiana,” alisema.

Aidha alizungumzia juhudi za kuleta uwiano baina ya jamii zainazoishi kwenye mipaka ya nchi husika, akitaja Uganda na Ethiopia kama mfano, ambapo Kenya na serikali za nchi hizo zilifikia makubaliano ya jinsi ya kufanya biashara kwa raia wa pande zote kwenye mipaka ya nchi hizo.

Lakini licha ya taarifa za kidiplomasia zinazotolewa na viongozi mara kwa mara kuhusu utangamano wa kieneo, wachambuzi wamemekuwa wakitilia shaka kama baadhi wa viongozi wa kanda ya Afrika Mashariki wana imani ya dhati na ushirikiano huo, licha ya mikakati ambayo imeendelea kupigiwa upatu na baadhi yao, mchakato ambao umekuwa ukiendelea kwa miongo kadhaa tangu kuvunjika kwa jumuiya ya zamani ya Afrika Mashariki mnamo mwaka wa 1976.

“Makosa yaliyotokea mnamo miaka ya sabini na ya sitini yaliyopelekea kuvunjika kwa jumuiya ya zamani ya Afrika Mashariki, bado yapo, na hali ya kutoaminiana bado ipo kwa kiasi fulani. Mimi nimekuwa katika msitari wa mbele nikisema kwamba yaliyopita si ndwele na tunaweza kujifunza kutokana na makosa yetu ya zamani,” aliongeza Kenyatta.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inazishirikisha nchi sita: Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Mkataba wa Kuanzishwa kwake ulitiwa saini tarehe 30 Novemba, 1999 na kuanza kutumika rasmi tarehe 7 julai, 2000 baada ya nchi Washirika kuuridhia.

Wakati wa mkutano huo wa Alhamisi, Rais Kenyatta pia alisisitiza kwamba hana nia ya kwendelea kuwa rais wa Kenya baada ya muhula wake wa pili kuisha, akisema kuwa Wakenya wanataka katiba, inayompatia kila rais mihula miwili ya mika mitano, iheshimiwe. Hata hivyo, alipoulizwa iwapo ana nia ya kuwa waziri mkuu baada ya kipindi chake cha urais kukamilika, kiongozi huyo alisema hana Habari kama kutakuwa na nafasi kama hiyo iwapo katiba itafanyiwa marekebisho.

XS
SM
MD
LG