Kesi ya ufisadi ya Rais wa zamani wa Afrika kusini Jacob Zuma imeanza tena kusikilizwa leo Jumatatu kufuatia siku kadhaa za ghasia zilizosababisha vifo kuhusiana na kesi tofauti zilizopelekea kufungwa kwake.
Zuma alionekana kwa njia ya video wakati kesi ikisomwa katika mahakama kuu ya Pietermaritzburg katika makazi ya rais huyo wa zamani kwenye jimbo la KwaZulu-Natal.
Anashtakiwa kwa makosa kadhaa ya ufisadi, ulaghai na ujambazi kuhusiana na mikataba mikubwa ya silaha ya mwaka 1999 iliyoshirikisha kampuni kubwa ya ulinzi ya Thales ya Ufaransa wakati alipohudumu kama makamu rais. Kampuni hiyo pia imeshtakiwa kwa ufisadi na utakatishaji fedha.
Zuma mwenye umri wa miaka 79 alijisalimisha kwa mashtaka katika jimbo analoishi, takribani wiki mbili zilizopita, kuanza kutumikia kifungo cha miezi 15 gerezani kilichotolewa na mahakama ya katiba mwishoni mwa mwezi Juni.
Hukumu hiyo ilikuwa ni kutokana na kutofika mbele ya uchunguzi juu ya ufisadi, wakati wa urais wake wa miaka tisa, ambao ulimalizika mwaka 2018.