Kampuni moja yenye makao yake nchini Marekani ambayo inafanya kazi kuhusiana na takwimu za kampeni ilithibitisha Jumamosi kwamba mkurugenzi wake alikamatwa Kenya na kufukuzwa nchini humo baada ya kufanya kazi na kampeni za upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wenye kinyang’anyiro kikali cha urais unaotarajiwa kufanyika Jumanne.
Kulingana na shirika la habari la Associated Press-AP kukamatwa kwa mkurugenzi wa kampuni ya Aristotle kumezusha wasi wasi zaidi kuhusu upigaji kura wa Agosti nane ikiwa ni siku kadhaa baada ya ofisa mmoja wa cheo cha juu kwenye kitengo cha mfumo wa mawasiliano katika tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC huko Kenya kupatikana akiwa ameteswa na kisha kuuwawa.
Brandi Travis wa Aristotle alisema Mkurugenzi John Aristotle Phillips raia wa Marekani na mfanyakazi mmoja raia wa Canada, Andreas Katsouris walikamatwa Ijumaa na walitakiwa kuondoka nchini humo leo Jumamosi. Travis alisema kwa sasa Phillips yupo kwenye ubalozi wa Marekani mjini Nairobi.
Watu hao wawili walikuwa wakimsaidia kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa masuala ikiwemo uchambuzi wa mkakati na takwimu na kwamba walichagua kujihusisha na uchaguzi wa Kenya kwa sababu walidhani kulikuwa na uwezekano wa kuwepo kasoro kadhaa kwenye uchaguzi huo, Travis aliiambia AP.