Kampuni ya kutengeneza dawa ya MODERNA imesema itaanzisha kituo cha utengenezaji wa bidhaa hiyo nchini Kenya ambapo kitakuwa ni cha kwanza Afrika kutengeneza chanjo ya RNA ikiwa ni pamoja na chanjo ya COVID 19.
Moderna imesema inatarajia kuwekeza kiasi cha dola milioni 500 katika kituo hicho nchini Kenya na kusambaza dozi milioni 500 za chanjo za Mrna kwa bara hilo kila mwaka .
Pia ina mpango wa kuanza kujaza dozi za chanjo yake ya COVID 19 barani Afrika mapema mwaka 2023. Afrika imekuwa nyuma sana kati ya maeneo mengine katika kutoa chanjo kwa raia wake kukabiliana na janga hilo na kumekuwa na juhudi kadhaa katika miezi ya karibuni kulisaidia bara hilo kutengeneza chanjo yake ya COVID 19.
“ Sote tunajua changamoto ambazo Kenya na bara zima la Afrika zilipitia katika hatua za awali za janga hili ambalo linasababisha Afrika kubaki nyuma. Sio kwa sababu ya kutaka bali ni kutokana na kukosa uzoefu na Moderna imekuja kujaza nafasi hiyo,” Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema katika taarifa.
Shirika la afya duniani mwaka jana lilianzisha kituo cha kuhamisha teknolojia nchini Afrika kusini ili kuyapa mataifa masikini uwezo wa kutengeneza chanjo za COVID 19 na imekuwa ikijaribu kupata dawa za kisasa na Pfizer kujiunga katika juhudi zake.