Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 20:23

Mwanamme anayeendesha kampeni kuhusu hedhi za wanawake nchini Kenya


Elimu kuhusu afya ya uzazi pamoja na masuala yanayofungamana na ngono ni baadhi ya mambo yanayoendelea kuzua gumzo pamoja na hisia mbalimbali katika jamii nyingi barani Afrika.

Kulingana na tamaduni nyingi za kiafrika, mijadala kama hii haipaswi kuzungumziwa hadharani huku wanaume wakikwepa kujihusisha na shughuli zinazowahusu wanawake moja kwa moja.

Hata hivyo vijana wengi Afrika Mashariki wanaonekana kuchangamkia harakati za kijamii kama njia mojawapo ya kutoa hamasa kuhusu mambo yanayogusa jamii.

James Atito ni kijana mwanaharakati kutoka Mombasa nchini Kenya ambaye amewashangaza wengi baada ya kuamua kujitosa katika kampeni ya kuangazia masuala ya hedhi kwa wasichana.

Atito anayefahamika kama “The Period Man” anasema alijitwika jukumu hilo baada ya kuona wasichana wengi wadogo wakipata tabu kwa kukumbwa na matatizo fulani wakati wa siku zao za hedhi.

“Kuna wakati nilienda sehemu inaitwa Turkana nikakuta wasichana wadogo wamekaa kwenye mitaro ya maji wakati wa hedhi na nilipowauliza wakasema hawakuwa na sodo za kujihifadhi wakati wa hedhi”anasema James Atito.

“Mimi mwenyewe nina dada yangu mdogo na nilipoona matukio kama yale niliguswa sana.” Atito aliongeza.

Kupitia kampeni yake ya “The Period Man”, Atito mwenye umri wa miaka 28 amekuwa akitembelea maeneo ya umma ikiwemo sokoni, shuleni pamoja na maeneo ya ibada na kuzungumza na wasichana huku pia akisambaza sodo taulo maalum ambazo hutumika wakati wasichana wakiwa katika hedhi.

PINGAMZI KUTOKA KWA JAMII.

Sio kawaida jamii kuona kijana mdogo wa kiume akijishughulisha na kampeni inayozungumzia masuala ya wanawake na hivyo Atito alipitia changamoto nyingi kabla jamii kumuelewa.

Watu wengi katika mji wa Mombasa na pwani ya Kenya kwa ujumla wameshikilia sana dini ya Kiislamu na imekuwa changamoto kwa Atito kueneza kampeni yake hasa katika maeneo ya umma.

“Watu wengi wananikashifu wakiniambia mimi kama mwanamme sifai kuzungumzia masuala ya hedhi, wengine wanasema dini hairuhusu” Anasema Atito.

“Kuna baadhi ya watu hasa wanawake na vijana hunishambulia kupitia mtandao wangu wa Facebook wakiniambia niwache ninachokifanya.” Anaongeza Atito ambaye mara nyingi akitembea huwa amebeba visodo kwenye mfuko.

WASICHANA WABADILISHA DHANA

Hadi kufikia sasa, mpango huo alioanzisha mwaka jana 2019 umefaulu kuwafikia takriban wasichana 2,000 katika pwani ya Kenya.

VOA Swahili imezunguma na Beatrice Adhiambo, mmoja kati ya wasichana wanaoendelea kufaidika na mpango huu wa “The Period Man.”

Beatrice ambaye ni mwanafunzi wa shule ya upili anasema kwa mara ya kwanza ilikuwa vigumu kujihusisha na mpango huo huku pia akishindwa kuzungumzia hali yake ya hedhi hadharani.

“Kabla sijajiunga na mpango huu nilikuwa nikiogopa sana kuzungumzia hali yangu ya hedhi hasa mbele ya wanaume, nilikuwa naona aibu lakini nimepata ufahamu mkubwa sasa” anasema Beatrice.

Mpango huu wa “The Period Man” nchini Kenya unajiri wanaharakati wa kijamii wanaoendelea kushinikiza serikali mbalimbali kuweka mikakati ya kuhakikisha bidhaa kama vile taulo za hedhi zinapatikana kwa urahisi.

Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa mmoja kati ya wasichana kumi katika eneo la Afrika kusini mwa janga la Sahara hukosa shule kila mara wakati wao wa hedhi na hivyo kuathiri masomo yao.

XS
SM
MD
LG