Mkuu wa idara ya kupambana na HIV na Ukimwi ya Umoja wa Mataifa-UNAIDS, Michel Sidibe alisema jumuia ya kimataifa ipo kwenye wakati muhimu katika juhudi za kumaliza janga la HIV na ukimwi ifikapo mwaka 2030.
Sidibe aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba wakati huu tukiwa kati kati ya juhudi zetu ni muhimu kutathmini kile ambacho kilikuwa hakifanyi kazi, akieleza kwamba mwaka huu ndio tunafika nusu ya njia za kufikia malengo yaliyokubaliwa kimataifa. Ni kuhusu namna ya kukabiliana na jamii zilizo hatarini, jamii dhaifu.
Kulingana na takwimu za 2016 watu milioni 36.7 duniani wanaishi na HIV. Kulikuwa na takribani watu milioni mbili wenye maambukizo mapya na vifo milioni moja vilivyohusiana na ukimwi. Lakini habari njema ni kwamba kumekuwa na mafanikio katika kupanua nafasi za kupata dawa za ARV ambazo ziliwafikia takribani watu milioni 21 mwaka 2016 na kupelekea kupunguza kwa theluthi moja ya vifo vilivyohusiana na ukimwi duniani.
Kutokomeza maambukizo ya HIV kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua na kunyonyesa limekua pia jambo linaloangaliwa kwa makini ifikapo mwaka 2030. Suala hili lilionekana kama ndoto miaka michache iliyopita, alisema Sidibe.