Tume ya uchaguzi nchini Uganda, ilitangaza matokeo kufuatia uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Jumatano ambao haukuwa na shamra shamra nyingi sana kama uchaguzi wa urais uliofanyika Februari 18 mwaka 2016.
Tume hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya Uganda ilitangaza matokeo rasmi ya kiti cha Meya katika jimbo la Kampala majira ya saa kumi na moja alfajiri siku ya Alhamis kwa saa za Uganda. Tume ilisema bwana Lukwago ndie mshindi wa kiti hicho.
Hatua hii ilifuatia kitisho kilichotolewa na baadhi ya vijana wa jiji la Kampala wengi wakiwa wafuasi wa chama cha upinzani ambao waliamini kwa njia moja au nyingine mgombea wao ndie mshindi katika uchaguzi huu.
Vijana hao walitoa vitisho vya kuchoma moto majengo kadhaa iwapo tume itachelewesha kutoa matokeo na kupelekea kutangaza matokeo ya uongo ya mshindi wa jimbo hilo huku tume ikifahamu ukweli kwamba upinzani ndio ulioshika nafasi ya juu katika jimbo la Kampala lenye wakazi wengi ambao ni wafuasi wa upinzani.
Sauti ya Amerika-VOA ilifanya mahojiano na mwandishi wake wa mjini Kampala, Kennes Bwire na kwanza kutaka kujua iwapo hili ni jambo la kawaida kwa tume ya uchaguzi nchini Uganda kutangaza matokeo yeyote ya uchaguzi saa za alfajiri.