Ghana imetuma wanajeshi 1,000 na polisi katika eneo la kaskazini la Bawku ili kuimarisha usalama baada ya watu wenye silaha kumuua afisa wa uhamiaji na kuwajeruhi watu wengine wawili karibu na mpaka na Burkina Faso wiki iliyopita maafisa wa serikali wamesema.
Bawku, eneo lililoko katika mkoa wa Upper East nchini Ghana, linakabiliwa na mzozo mkubwa wa kikabila ambapo mara nyingi ghasia zinazuka, pamoja na hatari inayoongezeka ya kusambaa mzozo wa kijihadi kwenye mpaka.
Idara ya Uhamiaji ya Ghana haikueleza chanzo cha shambulio hilo wiki iliyopita, lakini ilisema maafisa hao watatu hawakuwa kazini wakati watu wenye silaha walipofyatua risasi kwenye gari lao nje ya kituo cha polisi cha Bawku.
Palgrave Boakye-Danquah, msemaji wa serikali kuhusu utawala na usalama aliliambia shirika la habari la AFP Jumanne jioni kwamba vikosi maalum vya ziada vilipelekwa Bawku kama hatua ya tahadhari ya kulinda mipaka wakati vitisho vya ugaidi vikiongezeka katika eneo.