Mabingwa watetezi Ujerumani wametolewa katika mashindano ya fainali za kombe la dunia baada ya kufungwa 2-0 na Korea Kusini katika mechi yao ya mwisho ya Kundi E.
Hili litakumbukwa kama moja ya matukio makubwa ya fainali za Russia 2018 lakini pia ni muendelezo wa masahibu ya mabingwa watetezi katika miaka ya hivi karibuni. Mabingwa watetezi ambao walitolewa mapema katika miaka ya karibuni ni Ufaransa (2002), Italia (2010), Uhispania (2014) na sasa Ujerumani yamewakuta.
Wakati hayo yanawatokea Ujerumani, Mexico nayo ilichapwa 3-0 na Sweden. Matokeo hayo yakaamua timu mbili kutoka Kundi F kuingia raundi ya 16 kuwa ni Sweden ambayo ilimaliza na pointi sita, ikifuatiwa na Mexico ambayo nayo ilimaliza ikiwa na pointi sita. Ujerumani na Korea Kusini zilitoka katika mashindano kila moja ikiwa na pointi tatu.
Baada ya kufungwa 1-0 na Mexico katika mechi yao ya ufunguzi Ujerumani walijiweka vizuri kwa kushinda mechi yao iliyofuata 2-1 dhidi ya Sweden na kujipatia pointi tatu. Walihitaji ushindi dhidi ya Korea Kusini Jumatano kusonga mbele, hali ambayo ilikuwa inaoneka katika uwezo wa mabingwa hao watetezi.
Hata hivyo Wakorea ambao walikuwa wanachezea kutunza heshima yao tu - kwani hawakuwa na nafasi yoyote ya kusonga mbele - walikaza mkanda na kuwaweka mabingwa watetezi katika hali ngumu kwenye pambano zima.
Magoli yote ya Korea Kusini yote yalipatikana katika dakika za nyongeza huenda Wajerumani wakidhani kuwa watapata sare waliyokuwa wanatafuta. Kim Young-gwon alifunga katika dakika ya 93 na Son Heung-min akapachika bao la pili katika dakika ya 96.
Katika raundi ya pili Mexico na Sweden zitacheza na washindi wa kundi F.