Afrika Kusini wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia walianza mashindano hayo Ijumaa kwa kutoka sare 1-1 na Mexico katika mechi ya ufunguzi iliyokuwa na kandanda la kusisimua kabisa baina ya timu hizo mbili. Katika mechi ya pili ya kundi A Ijumaa Ufaransa na Uruguay zilitoka sare 0-0 katika mechi ambapo Uruguay walimaliza mchezo wakiwa wamebakiwa na wachezaji kumi tu baada ya mchezaji wao mmoja kupigwa kadi nyekundu.
Winga wa Afrika Kusini Siphiwe Tshabalala alifunga goli la kwanza katika fainali za mwaka huu katika dakika ya 55 katika uwanja wa Soccer City. Lakini mlinzi wa Mexico Rafael Marquez alipata bao la kusawazisha katika dakika ya 79 ya mchezo.
Matokeo hayo yanazipa zote Afrika Kusini na Mexico pointi moja moja kutoka katika kundi A. Na pia matokeo hayo yameendeleza kawaida ya kombe la dunia ambapo timu wenyeji wa mashindano hawajawahi kupoteza mechi ya kwanza ya fainali hizo. Afrika Kusini sasa ina kazi ya kuhakikisha inavuka kuingia raundi ya pili.
Nafasi ya Afrika Kusini imekuwa nzuri pia baada ya mechi ya pili ya kundi hilo kati ya Uruguay na Ufaransa kutoka sare 0-0. Matokeo hayo yana maana kuwa timu zote katika kundi A zina pointi moja moja lakini Afrika Kusini na Mexico zinashika nafasi mbili za juu kwa sababu kila timu ina goli moja.