Umoja wa Ulaya siku ya Jumapili uliitaka Russia kubadili uamuzi wake wa kujiondoa katika makubaliano ya nafaka yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, hatua ambayo ilidhoofisha juhudi za kupunguza mzozo wa chakula duniani, na kwamba Ukraine ilisema Moscow ilipanga hivyo mapema sana.
Moscow ilisitisha ushiriki wake katika makubaliano ya Black Sea siku ya Jumamosi na kupunguza usafirishaji kutoka Ukraine moja ya wauzaji wakuu wa nafaka duniani kujibu kile ilichokiita shambulizi kubwa la ndege zisizo na rubani za Ukraine mapema siku hiyo kwenye meli yake karibu na bandari ya Sevastopol huko Crimea eneo linalokaliwa kimabavu na Russia.
"Uamuzi wa Russia wa kusitisha ushiriki katika makubaliano ya Black Sea unaweka katika hatari njia kuu ya usafirishaji wa nafaka na mbolea ili kushughulikia mgogoro wa chakula duniani unaosababishwa na vita vyake dhidi ya Ukraine," mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema kupitia ukurasa wake wa Twitter.
"EU inaitaka Russia kubadilisha uamuzi wake."
Siku ya Jumamosi, Rais wa Marekani Joe Biden aliitaja hatua hiyo kuwa "ya kukasirisha sana" akisema itaongeza njaa, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa marekani, Antony Blinken aliishutumu Moscow kwa kutumia chakula kama silaha. Siku ya Jumapili, balozi wa Russia mjini Washington, aliijibu Washington, akisema jibu la Marekani lilikuwa "la kukasirisha” na kutoa madai ya uwongo juu ya hatua hiyo ya Moscow.