Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 14:27

EAC yashauriwa kuimarisha mikakati ya kuboresha uchumi


Naibu katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM) Chiristopher Bazivamo (kushoto) Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regina Hess (katikati) na Daniel Malanga (Kulia), mkurugenzi wa uchumi kwenye mamlaka ya usafiri wa angani ya Tanzania.
Naibu katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM) Chiristopher Bazivamo (kushoto) Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regina Hess (katikati) na Daniel Malanga (Kulia), mkurugenzi wa uchumi kwenye mamlaka ya usafiri wa angani ya Tanzania.

Serikali ya Ujerumani Jumatatu ilizishauri nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, EAC, kuimarisha mikakati ya pamoja ya kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na janga la Corona hasa katika sekta ya utalii.

Ujumbe huo uliwasilishwa Jumatatu na balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regina Hess wakati akizungumza na maafisa wa ngazi za juu kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro nchini Tanzania waliokuwa katika mafunzo maalum ya ya namna ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Regina alisema licha ya kuwepo kwa taarifa za kuanza kupungua ama kudhibitiwa kwa maambukizi ya virusi vya Corona katika baadhi ya nchi za Ukanda huo ikiwemo Tanzania, changamoto bado ni kubwa na ushirikiano zaidi unahijika.

Kuhusu hali ilivyo katika nchi wanachama kwa ujumla , naibu Katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika mashariki anayeshughulikia huduma za jamii Chiristopher Bazivamo alisema jitihada zinazofanywa na kila nchi kukabiliana na tatizo hilo zinaendelea kuonyesha mafanikio.

Baadhi ya wadau wanaosaidia nchi za Jumuiya hiyo akiwemo Bi Irine Lucassowitz kutoka shirika la maendeleo la Ujerumani GIZ walisema pia kuna haja ya baadhi ya nchi za jumuiya hiyo kuangalia upya njia zinazotumika kukabiliana na virusi vya Corona zikiwemo kufunga mipaka ambayo inaweza kuwa na faida na pia hasara kulingana na nchi husika na mfumo wa maisha ya wananchi.

Aidha serikali ya Ujerumani, kupitia shirika lake la maendeleo la GIZ, imetoa Euro laki tano kwa nchi wanachama wa jumuiya ya hiyo, ili kuimarisha usalama katika viwanja vya Ndege vinavyotumika zaidi kutoa mafunzo ambayo hadi sasa yameshatolewa kwa maafisa wa viwanja mbalimbali vya Ndege katika nchi wanachama.

-Imetayarishwa na Asiraji Mvungi, mwandishi wa VOA, Arusha, Tanzania

XS
SM
MD
LG