Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 15:14

Bunge la Somalia lapiga kura ya kuongeza muda wa rais na serikali yake


Wabunge wa Somalia wakipiga kura kuongeza muda wa rais Farmajo.
Wabunge wa Somalia wakipiga kura kuongeza muda wa rais Farmajo.

Siasa za Somalia ziliingia katika hali ya mkanganyiko Jumatatu wakati mabaraza mawili ya bunge yalipingana vikali juu hadhi ya Rais Mohamed Abdullahi Farmajo.

Baraza kuu la bunge lilipiga kura ya kuongeza muda wa rais na serikali yake kwa miaka miwili, wakati baraza jingine la bunge limesema hatua hiyo ilikuwa kinyume na katiba.

Kikao hicho maalum kilishuhudia wabunge 149 wakipigia kura pendekezo hilo la kuongezewa muda, huku watatu wakipinga.

Lakini ndani ya dakika chache, baraza jingine la bunge lilipinga, na spika akisema hatua ya baraza kuu ni kinyume na katiba.

Kwa vyovyote vile, hakuna ishara yeyote kwamba uchaguzi wa bunge na urais uliocheleweshwa wa Somalia utafanyika wakati wowote hivi karibuni.

Uchaguzi, ambao hapo awali ulipangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka jana, bado haujafanyika kwa sababu ya mabishano kati ya viongozi wa kisiasa juu ya nani atadhibiti mchakato wa uchaguzi.

Mazungumzo ya kumaliza mchakato huo yalimalizika kwa mkwamo licha ya shinikizo kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na washirika wengine wa kimataifa wa serikali ya Somalia.

Spika wa bunge, Mohamed Mursal, alisema Jumatatu kwamba wabunge lazima wawajibike kama wawakilishi wa watu, kuchukua maamuzi wakati mahitaji yanapotokea.

Rais Farmajo, ambaye muda wake madarakani ulimalizika rasmi Februari 8, mara moja alikubaliana na kuidhinishwa kuongezewa muda na baraza kuu la bunge.

Katika taarifa, rais aliwasihi raia kuchukua fursa ya kihistoria kuchagua hatima yao ya kidemokrasia.

Hata hivyo, wapinzani, wakiongozwa na waziri mkuu wa zamani, Hassan Ali Khaire, walionya kwamba kuongeza muda wa rais kunaweza kuwa na matokeo mabaya.

Hapo awali, mkuu wa polisi nchini humo Abdi Mohamed Hassan alimfukuza kazi kamanda wa polisi wa mkoa wa Mogadishu Jenerali Sadik Omar baada ya kujaribu kusimamisha kikao cha bunge, akitaja wasiwasi wa usalama.

XS
SM
MD
LG