Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, tangazo hilo limetolewa Jumatatu likiruhusu noti za zamani za naira 200, 500 na 1,000 kuendelea kutumika hadi Desemba 31. Msemaji wa Benki Kuu Isa Abdulmumin amesema kwamba hatua hiyo ilikusudiwa kufuata agizo la mahakama ya juu, iliyoamuru kwamba uzinduzi wa program hiyo ulikuwa kinyume cha sheria.
Jumanne noti mpya na za zamani zilikuwa bado hazipatikani kwa maelfu ya wateja waliokuwa wamepanga foleni nje ya mabenki kwenye mji mkuu Abuja. Nigeria imeshuhudia uhaba wa fedha kutokana na uchapishaji mdogo wa noti mpya zilizokuwa zitumike. Wachambuzi wanailaumu serikali kwa kuzindua sera hiyo kwenye taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, ambako mfumo wa malipo ya kidijitali haujafikia viwango vya kutegemewa. Kulingana Benki ya Dunia, ni asilimia 45 pekee ya watu wanaomiliki akaunti za benki.
Kituo cha kuimarisha biashara binafsi chenye makao yake mjini Lagos kimesema kwamba uchumi wa Nigeria umepoteza takriban naira trilioni 20 ambazo ni sawa na dola bilioni 43 za kimarekani. Kituo hicho kimeongeza kusema kwamba uhaba wa sarafu umeathiri biashara na watu binafsi kwenye taifa hilo ambalo asilimia 63 ya watu ni maskini, huku asilimia 33 wakiwa hawana ajira.