Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 12:14

Ajali za barabarani- wajibu wa madereva


Kila nchi ya Afrika Mashariki ina vigezo walivyowekewa madereva ili kuruhusiwa kuendesha magari ya abiria na hata ya mizigo. Hali ni hiyo hiyo kwa magari yenyewe kutembea barabarani.

Hii ni pamoja na usafiri wa pikipiki, maarufu kama bodaboda, ambazo zimezidi kuongezeka katika siku za hivi karibuni kwenye eneo lote la Afrika Mashariki.

Mamlaka za kuratibu maswala ya usafiri, zinafafanua lengo la vigezo hivi ni kuhakikisha kwamba usalama upo barabarani.

Nchini Kenya, Mamlaka ya usafiri, National Transport and Safety Authority, NTSA, ambayo ndiyo iliyotwikwa jukumu la kutoa vyeti vya kuendesha magari, imeeleza bayana majukumu ya madereva kabla ya kuruhusiwa kuendesha gari au hata chombo chochote cha abiria.

Mamlaka hiyo iliyo anzishwa mnamo mwaka wa 2012, imekuwa ikifanya kampeni za mara kwa mara kuwahamasisha madereva, wenye magari na abiria, kuhusu umuhimu wa kuzingatia kanuni za usalama wa barabarani.

Mwanasarakasi na mchekeshaji maarufu nchini Kenya Charles Bukeko, akiigiza katika moja ya kampeni hiyo kupitia mtandao wa Youtube, anaeleza kwamba madereva wasio heshimu ishara za barabarani wanaendelea kusababisha maafa katika barabara za nchi hiyo, ameelezea zaidi.

Je ni masharti gani wanayopewa madereva kabla ya kuruhusiwa kuendesha magari haya? Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa magari ya abiria nchini Kenya; Matatu Owners Association, Simon Kimutai, anasema kuwa hatua ya kwanza ni kuwapa madereva mafunzo ya kutosha.

Ameongeza kwamba baadhi ya madereva hawapati ujuzi kabla ya kuanza kuendesha magari ya abiria, licha ya kuwa na leseni. Wengine, anasema, hujifunza udereva vichochoroni bila ya kwenda shule zinazotoa mafunzo hayo.

Lakini kwa mujibu wa maelezo ya Kimutahi, sio madereva wote wanafuata taratibu zilizowekwa na mamlaka hiyo ya NTSA.

Kwa mfano anaeleza kwamba madereva wengine huvifanyia ukarabati vyombo vya kudhibiti mwendo, kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

Naye makamu wa mwenyekiti wa chama cha wasafirishaji cha Tanzania, Omari Said Kiponza anaeleza vigezo vya madereva kuweza kupata leseni nchini Tanzania.

Akihojiwa na mwandishi wa Sauti ya Amerika mjini Dar es Salaam, George Njogopa, Kiponza amesema kuwa madereva wanalazimika kuonyesha cheti cha kudhibiti vyombo vya usafiri kabla ya kuajiriwa.

Nchini Uganda, hali si tofauti sana na nchi jirani. Ingawa sheria zinaeleza wajibu wa madereva na kuweka vigezo vinavyopasa kufuatwa na magari ya abiria na vyombo vingine vya usafiri.

Kadhalika ripoti ya shirika la Afya Duniani (WHO), inaeleza kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani iko juu kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki. Takwimu zinaonyesha kuwa kuna asilimia 27.4 ya vifo kati ya kila watu laki moja kila mwaka.

Hii ina maana kwamba madereva wengi hawafuati sheria za barabarani na kwamba kuna ulegevu wa utekelezaji wa majukumu kwa vyombo vinavyohusika na usalama nchini humo, ikiwa ni pamoja na polisi na mahakama.

Wasanii mbali mbali wamelazimika kutunga nyimbo, kama njia ya kuwakumbusha madereva juu ya umuhimu wa kutii sheria barabarani.

Nchini Tanzania, Kenya na Uganda, sheria zinazo wahitaji madereva, hususan wanaoendesha malori au mabasi kwa muda mrefu, kupumzika kabla ya kwendelea na safari, hazifuatwi na madereva wengi. Hali hii imetajwa kama moja ya sababu za ongezeka la ajali kwenye barabara za nchi hizo. Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa Magari nchini Kenya amesema:

“Licha ya baadhi ya idara husika za serikali kuweka mikakati na kanuni za kufuatwa na madereva ili kujaribu kupunguza ajali za barabarani katika eneo la Afrika Mashariki.”

Amesema inaoneka kuwa, wengi wa madereva na hata wenye magari huzikumbuka tu kanuni hizo kunapotokea ajali mbaya na watu kupoteza maisha yao. Baada ya kuzungumziwa kwa siku chache, ajali hizo pia husahaulika haraka na maisha kuendelea kama ilivyokuwa kabla ya ajali hizo kutokea….yaani hadi pale ajali nyingine itagonga vichwa vya habari kwenye vyombo vya habari.

Licha ya kuonekana kuwa watu wanasahau haraka na kuanza tena kupuuza sheria za barabarani, kuna umuhimu wa kuimarisha utekelezaji wa sheria hizo, ili kupunguza maafa na hasara itokanayo na ajali hizo ambazo nyingi kati ya hizo zinaweza kuepukwa.

XS
SM
MD
LG