Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameliamuru jeshi lake, kitengo cha silaha na sekta ya silaha za nyuklia kuharakisha maandalizi ya vita ili kukabiliana na kile alichokiita hatua za mapambano ambazo hazijawahi kufanywa na Marekani, vyombo vya habari vya serikali vimesema Alhamisi.
Akizungumza kuhusu mwelekeo wa sera ya mwaka mpya katika mkutano muhimu wa chama tawala nchini humo siku ya Jumatano, Kim pia alisema Pyongyang itapanua ushirikiano wa kimkakati na nchi “zinazopinga utawala wa kibeberu”, shirika la habari la KCNA liliripoti.
“Aliweka majukumu ya wanamgambo wa People’s Army na sekta ya silaha, silaha za nyuklia na sekta za ulinzi wa raia ili kuongeza kasi ya maandalizi ya vita,” KCNA ilisema.
Korea Kaskazini imekuwa ikipanua uhusiano wake na Russia, miongoni mwa mengine, huku Marekani ikiishutumu Pyongyang kwa kusambaza vifaa vya kijeshi kwa Moscow kwa ajili ya matumizi yake katika vita vyake na Ukraine, wakati Russia ikitoa msaada wa kiufundi kusaidia Korea Kaskazini kuendeleza uwezo wake wa kijeshi.
Forum