Mabomu ya ndani ya gari yamewaua watu wasiopungua wanane wakiwemo watoto watatu katika matukio mawili tofauti siku ya Jumapili kaskazini mwa Syria, shirika linalofuatilia masuala ya vita limesema.
Mlipuko mmoja ulipiga katika duka la kutengeneza magari huko Shawa, kijiji kilicho karibu na mpaka wa Uturuki unaoshikiliwa na wapiganaji wanaoiunga mkono Ankara, wakaazi waliliambia shirika la habari la AFP. Raia watano wakiwemo watoto watatu waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa, shirika linalofuatilia haki za binadamu kwa Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema.
Maeneo yanayoshikiliwa na Uturuki na washirika wake wa Syria huko kaskazini mwa Syria ni eneo linalotokea mauaji ya mara kwa mara, mabomu na mapigano kati ya makundi yenye silaha. Katika tukio la pili, kifaa chenye mlipuko kilichotegwa ndani ya gari kiliwaua wapiganaji watatu wenye uhusiano na kikosi cha Kikurdi cha Syrian Democratic Forces (SDF) katika mji wa Manbij, kulingana na shirika la uangalizi wa haki za binadamu.
Manbij ni ngome ya zamani ya kundi la Islamic State ambalo kwa sasa linashikiliwa na baraza la kijeshi lenye uhusiano na SDF linaloungwa mkono na Marekani. Hakukuwa na madai ya haraka ya kuhusika na mashambulizi hayo.
Forum