Takribani raia 35 waliuawa na 37 walijeruhiwa kaskazini mwa Burkina Faso siku ya Jumatatu wakati gari lililokuwa kwenye msafara lilipokanyaga bomu lililotegwa barabarani.
Serikali ya mpito ilisema katika taarifa kwamba Msafara wa ugavi uliosindikizwa kuelekea mji mkuu Ouagadougou ulikanyaga bomu hilo kati ya miji ya kaskazini ya Djibo na Bourzanga eneo ambalo wanamgambo wa Kiislam wameongeza mashambulizi dhidi ya vijiji, polisi na kambi za wanajeshi wa nchi za nje tangu mwaka 2015.
Walinzi waliofuatana na msafara huo walilinda eneo hilo haraka na kuchukua hatua za kuwasaidia waathiriwa, serikali ya kijeshi ilisema katika taarifa. Ukosefu wa usalama umeongezeka katika kanda ya sahel huko Afrika magharibi mnamo muongo mmoja sasa huku makundi yenye uhusiano na makundi ya al-Qaida na Islamic State (IS) yakizidi kupata nguvu na kuua maelfu ya watu na kuwalazimisha zaidi ya watu milioni moja kuyahama makazi yao licha ya kuwepo kwa wanajeshi wa kigeni na walinda amani wa Umoja wa Mataifa.
Hasira kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi kulichochea mapinduzi ya kijeshi dhidi ya rais wa zamani wa Burkina Faso, Roch Kabore hapo mwezi Januari.