Somalia iliishutumu kenya kwa kukiuka mamlaka yake ya kujitawala baada ya mwakilishi wa eneo lililojitenga la Somaliland kualikwa Jumanne kwenye mkutano wa kidiplomasia mjini Nairobi.
Balozi wa Mogadishu mjini Nairobi Mohamoud Ahmed Nur alitoka nje ya tukio hilo akipinga uwepo wa mjumbe wa Somaliland ubalozi wake ulisema katika taarifa.
Mzozo huo unakuja siku chache baada ya kiongozi wa kenya, Uhuru Kenyatta alipohudhuria sherehe za kuapishwa Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akiashiria kuboresha zaidi uhusiano ambao mara nyingi umekuwa na dosari.
Somalia pia ilikubali kuanza tena uagizaji wa miraa kutoka Kenya baada ya kupigwa marufuku kwa miaka miwili kama sehemu ya mkataba mpana wa kibiashara unaofanywa kati ya majirani wa Afrika mashariki.
Mogadishu ilikuwa imevunja uhusiano wa kidiplomasia Disemba mwaka 2020 baada ya Nairobi kuwa mwenyeji wa uongozi wa kisiasa wa Somaliland lakini walikubali kurejesha uhusiano mwezi Agosti mwaka 2021.