Uingereza imefuta safari ya ndege iliyokuwa imepangwa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda siku ya Jumanne jioni baada ya mahakama ya ulaya ya haki za binadamu kuingilia kati ikisema mpango huo ulikuwa hatari ya kweli kwa madhara ambayo yasiyoweza kutenguliwa.
Uamuzi wa kufuta safari ya ndege ulitokana na siku tatu za changamoto kali za mahakama, kutoka kwa mawakili wa haki za wahamiaji ambao waliwasilisha msururu wa rufaa za kesi baada ya kesi wakitaka kuzuia kuondolewa kwa kila mtu aliyekuwa kwenye orodha hiyo ya serikali.
Maafisa wa serikali ya Uingereza walisema mapema Jumanne kwamba ndege hiyo ingeondoka bila kujali ni watu wangapi waliokuwemo ndani. Vyombo vya habari vya uingereza viliripoti kuwa idadi ya watu wanaotarajiwa kufukuzwa ilikuwa zaidi ya 30 siku ya Ijumaa.
Baada ya safari ya ndege kufutwa, waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Priti Patel alisema alisikitishwa lakini hatazuiliwa kufanya jambo sahihi. Aliongeza kuwa timu yetu ya sheria inakagua kila uamuzi uliofanywa kwenye safari hii ya ndege na maandalizi ya safari ya pili ya ndege yanaanza hivi sasa.