Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 16:54

Mahakama kuu Kenya imesitisha kwa muda utekelezaji wa sheria ya usawa wa jinsia kwa vyama vya kisiasa


Mahakama Kenya imesitisha kwa muda sheria ya usawa wa jinsia
Mahakama Kenya imesitisha kwa muda sheria ya usawa wa jinsia

Mahakama kuu nchini Kenya imesitisha kwa muda utekelezaji wa sheria ya usawa wa jinsia inayovitaka vyama vyote vya kisiasa vinavyotaka kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 9 viwasilishe usajili wa wagombea kwa kuzingatia sheria hiyo inayosisitiza kwamba jinsia moja hairuhusiwi kupata zaidi ya theluthi mbili ya viti vya bunge.

Jaji Anthony Ndung’u alitoa agizo hilo kufuatia ombi la wakili Adrian Kamotho ambaye anapinga uhalali wa uamuzi wa tume hiyo kutekeleza sheria hiyo.

Jaji Antony Ndung’u wa mahakama kuu nchini Kenya ameeleza kuwa Kamotho amedhihirisha masuala mazito yanayohitaji kusikilizwa upesi katika kesi yake inayopania kudhibiti tume ya uchaguzi IEBC kutekeleza sheria hiyo inayovilazimisha vyama vya kisiasa nchini Kenya kufikia Alhamisi kuwasilisha sajili ya wagombea isiyoruhusu jinsia moja kupata zaidi ya theluthi mbili ya viti vya bunge.

Katika uamuzi wake unaotoa nafasi kwa kesi hiyo kuendelea kusikilizwa siku tatu baada ya tume ya uchaguzi kuongeza muda kwa vyama vya kisiasa kutimiza mahitaji ya sheria hiyo la sivyo visiruhusiwe kuwa na wagombea katika uchaguzi mkuu Jaji Ndung’u ameeleza kuwa ameshawishika kuwa Bw Kamotho ametoa hoja zinazowiana na sheria.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati wiki hii alieleza kuwa baadhi ya vyama vya kisiasa vilivyo na wagombea wengi havijawasilisha sajili inayozingatia sheria hiyo na hata baada ya kupewa muda zaidi hadi Mei tarehe 9 kurekebisha na kuwasilisha sajili inayozingatia sheria hiyo ya theluthi mbili, bado havijafuata sheria.

Kamotho katika kesi yake mbele ya mahakama hiyo ameeleza kuwa mahitaji ya IEBC kulazimisha vyama vya kisiasa kutimiza masharti ya sheria hiyo ya jinsia ni ya kibaguzi na ina nia ya kuviacha nje vyama vya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu.

Aidha wakili huyo anakariri kuwa IEBC kuendelea kusisitizia utekelezaji wa sheria hiyo ni uonevu mkubwa na juhudi zisizokuwa na maana kwa mfumo wa kidemokrasia nchini Kenya na kuitaka mahakama kudhibiti utekelezaji wa sheria hiyo.

Vyama vya kisiasa nchini Kenya vinakabiliwa na ugumu wa kutimiza mahitaji ya usawa wa jinsia katika sajili zake za wagombea watakaowania nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika uchaguzi huo wa Agosti 9 baada ya tume ya uchaguzi IEBC kukariri kuwa sheria hiyo ni sharti itimizwe baada ya vyama hivyo kufanya kura ya mchujo kuwapata wagombea.

Tume hiyo imevionya vyama vya kisiasa kuwa itatupilia mbali orodha ya wagombea kutoka chama fulani cha kisiasa iwapo idadi ya wagombea wa kiume ni wengi mno kupita kiasi kinachohitajika kuliko idadi ya wagombea wa kike.

Wakili wa mahakama kuu Danstan Omari anaeleza kuwa mahakama kwa sasa inayapa kipaumbele masuala yanayofungamana na uchaguzi wa Agosti 9 na kwa kiasi kikubwa huenda isiathiri kalenda ya matayarisho ya IEBC.

IEBC inaeleza kuwa ikitokea chama cha kisiasa kitawasilisha orodha wa wagombea 290 wa nafasi ya ubunge kulingana na nafasi za kuchaguliwa si zaidi ya wagombea 193 wanastahili kuwa wa jinsia moja.

Pia ikitokea kuwa chama cha kisiasa kitawasilisha orodha inayojumuisha wagombea 47 wa bunge la Seneti si zaidi ya wagombea 31 wanastahili kuwa wa jinsia moja.

Vile vile ikitokea kuwa chama cha kisiasa kitawasilisha orodha inayojumuisha wagombea wasiofikia idadi ya maeneo yanayogombewa, sheria ya jinsia moja bado itatumika.

XS
SM
MD
LG