Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Alhamis aliidhinisha msaada mwingine wa kijeshi wa Marekani wa dola milioni 800 kwa Ukraine akitangaza ilikuwa muhimu kuvisaidia vikosi vya Kyiv kuwafukuza wapiganaji wa Russia katika vita ibaya vinavyoendelea katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Msaada huo unajumuisha silaha nzito za kivita, darzeni za bunduki za kurusha makombora na risasi 144,000. Biden alisema katika hotuba fupi huko White House kwamba shehena hiyo mpya ya silaha ililenga hasa kuvisaidia vikosi vya Ukraine kupigana katika eneo la Donbas ambalo ni tambarare zaidi, ardhi yake ipo wazi kuliko ambako mapigano ya awali yaliyotokea huko magharibi.
Biden alisema msaada huo mpya pamoja na msaada mwingine wa dola milioni 800 uliotangazwa wiki iliyopita, unakaribia kumaliza idhni ya bunge ya msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine. Lakini Rais Biden alisema karibuni ataliomba bunge pesa zaidi kwa ajili ya vikosi vya Ukraine.
Rais Biden alisema Marekani na washirika wake wa Magharibi bado wameungana katika azimio lao la kuisaidia Ukraine kupigana katika maeneo yake dhidi ya uvamizi wa wiki nane wa Rais wa Russia Vladmir Putin.