Meya wa New York Eric Adams, ametoa taarifa ya video kupitia ukurasa wa Twitter, akiwataka wakazi wa jiji hilo kutoa habari zozote zitakazo saidia uchunguzi kuhusiana na shambulizi la bunduki kwenye treni ya chini kwa chini ya jiji hilo siku ya Jumanne asubuhi.
Katika ujumbe wake Adams, anasema kwamba, "Ninawaombea wakazi wote wa New York walojeruhiwa kutokana na shambulio la leo kupata afweni ya haraka."
Mshambuliaji aliyefunika uso, alilipua bomu la kutoa moshi na kuanza kufyetua risasi ndani ya treni ya jijini New York ambapo watu 16 walijeruhiwa na kusababisha taharuki wakati wa harakati nyingi asubuhi.
Kamishna wa polisi wa New York, Keechant Sewel, amewaambia waandishi habari kwamba uchunguzi umeanza lakini shambulio hilo halichukuliwi kuwa ni la kigaidi.
Aliwahakikishia wakazi wa New York kwamba hakuna bomu lolote liliopatikana kwenye mfumo wa usafiri wa treni za chini kwa chini na kwamba wako katika hali ya juu ya usalama.
Sewell anasema mshambuliaji hajapatikana bado na hawafahamu sababu zake za shambulio hilo.