Mwanadiplomasia wa juu wa Umoja wa Ulaya ameamuru kusitishwa kwa mafunzo ya kijeshi kwa wanajeshi nchini Mali. Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa ulaya Josep Borell anataka kuhakikishiwa dhamana kutoka kwa serikali huko kwamba wakufunzi hao hawatafanya kazi na mamluki wa Russia.
Jumuiya hiyo yenye mataifa 27 imekuwa ikitoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali tangu mwaka 2013. Ilikuwa imepanga kuendelea kufanya hivyo licha ya hali ya wasi wasi na musikosuko ya kisiasa iliyoikumba nchi hiyo yakiwemo mapinduzi ya hivi karibuni ya kijeshi.
Lakini EU ina wasiwasi mkubwa kwamba utawala wa kijeshi una maelewano na mamluki wa Wagner Group. Borrell alisema Jumatatu kwamba EU inapaswa kuendelea na kazi za mafunzo pekee ambazo hazihusiani moja kwa moja na utoaji mafunzo kwa wanajeshi wa Mali katika mapambano ya kijeshi.