Kulingana na matokeo yanayotangazwa na vyombo vya habari vya Marekani, Biden anaonekana kua mshindi mkubwa katika uchaguzi wa awali ulofanyika Jumanne Marchi 10, 2020.
Uchaguzi huo unafuatia uchaguzi wa awali wiki moja iliyopita unaofahamika kama "Super Tuesday" katika majimbo 14 ambapo Biden alipata ushindi katika majimbo 10 huku Sanders akishinda katika majimbo manne.
Matokeo hayo yamempatia makamu rais wa zamani wajumbe 713 kati ya wajumbe 1,991 wanaohitajika ili kuchaguliwa kuwa mgombea kiti cha rais kwa tiketi ya chama cha Demokratik wakati wa uchaguzi mkuu wa Disemba.
Seneta Bernie Sanders, aliyekua anaongoza katika uchunguzi wa maoni hadi Jumanne wiki iliyopita amepatwa na pigo jingine kubwa wiki hii baada ya kushindwa katika "Super Tuesday, na wachambuzi wanasema itakua vigumu kwake yeye kuweza kumfikia Biden hivi sasa akiwa na wajumbe 589 kabla ya uchaguzi huu wa Jumanne.