Rais Barack Obama anasema, dunia ina jukumu la pamoja katika kuzuia maafa yaliyotokea Hiroshima kutokea tena, alipokua anatoa heshima zake kwa waathiriwa wa bomu la nuklia lililodondoshwa katika mji huo miongo saba iliyopita.
"Tunasimama hapa kati kati ya mji huo na tunajilazimisha kufikiria na kuwaza hali ilikuaje bomu lilipodondoka.", alisema Rais Obama siku ya Ijumaa akiwa Bustani ya Amani ya Hiroshima.
Obama ni rais wa kwanza wa Marekani aliye madarakani kutembelea mji wa Hiroshima tangu shambulio hilo la kumaliza vita vya pili vya dunia.
Akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, Obama alifungua ukurasa mwengine wa kihistoria alipotembelea bustani hiyo ya makumbusho na kukutana na baadhi ya walonusurika na shambuliop la kwanza la nuklia duniani.
Takriban watu 140,000 walifariki Hiroshima pale ndege ya kimarekani ilipodondosha bomu Agosti 6, 1945 na wengine 74,000 walifariki siku mbili baadaye katika mlipuko wa pili katika mji wa Nagasaki.
Katika hotuba yake Obama alitoa wito kwa watu kutowasahao waathiriwa wa Hiroshima na kutaka kuwepo na muelekeo mpya kuhusiana na silaha za nuklia.