Ujumbe wa mabalozi wa Umoja wa Ulaya EU pamoja na balozi wa Marekani mjini Kampala wamekutana na kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye nyumbani kwake Kasangat siku ya Ijumaa.
Ujumbe huo uloongozwa na balozi wa EU nchini Uganda Bw. Kristian Schmidt, ulizuiliwa kwanza na polisi kuingia nyumbani kwa kiongozi wa chama cha Forum for Democratic Change FDC, hadi kuwasili kwa mkuu wa idara ya kuajiri watu katika polisi Bw. Felix Andrew Kaweesi.
Akizungumza baada ya mkutano wao Bw Schmidt amesema lengo la mkutano ni kujadili masuala matatu muhimu. Kuendelewa kushikiliwa kwa Besigye nyumbani kwake na vituo vya polisi, uwezekano wa kuwasilisha mashtaka mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi na utumiaji wa lugha inayoweza kuchochea ghasia.
Ujumbe huo wa Mabalozi umetoa wito pia kwa serikali ya Kampala kutomweka mateka Besigye nyumbani kwake na kuheshimiwa haki zake za binadam.
Umoja wa Ulaya siku ya Alhamisi uliitaka tume ya uchaguzi ya Uganda kutoa maelezo kamili ya matokeo ya uchaguzi wa rais ulofanyika terehe 18 February.
Siku ya Jumanne ujumbe ya ufuatiliaji uchaguzi ya EU ulitembelea ofisi za FDC katika juhudi za kukusanya ushahidi wa kasoro na wizi wa kura wakati wa uchaguzi huo wa rais.