Rais Salvar Kiir wa Sudan Kusini amemteua hasimu wake, kiongozi wa waasi Riek Machar, kua makamu rais wa kwanza. Taarifa ya Rais Kiir iliyotangazwa Alhamisi na msemaji wake ni moja wapo ya hatua za kutekeleza makubaliano ya Amani ya Addis Ababa ya Ogusti 2013.
Uteuzi huo wa Machar unarudisha kwa sehemu kubwa utawala ulokuwepo kabla ya kuzuka kwa vita kati ya majeshi ya viongozi hao wawili hapo Disemba 2013, isipokua hivi sasa kutakuwepo na serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa
Akizungumza na Sauti ya Amerika Riek Machar anasema alishtushwa na tangazo hilo kwani hakutegemea rais atachukua uwamuzi huo wakati huu aloueleza ni "hatua ya kishuja", hata hivyo alimshukuru na kumpongeza. .
"Kwa maoni yangu ninadhani hatuna njia nyengine isipokua kutekeleza makubaliano ya Addis Ababa, kwani wananchi wa Sudan Kusini wamekumba na maafa ya kutosha. Hata baada ya makubaliano yalipotiwa saini kulikuwepo na mapigano ya hapa kwa pale na ni matumaini yangu uhasama huu utamalizika," alisema Machar
Tofauti kuu hivi sasa katika mfumo wa utawala huko Juba ni kwamba Machar anaruhusiwa kuleta wanajeshi wake wa kundi lake la SPLM ili kuweza kuunda jeshi moja la taifa.
Akizungumzia vipau mbele vyake baada ya kuwasili Juba, Bw Machar anasema cha kwanza ni kiukamilisha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
"Ni muhimu pia kuhakikisha amani inadumishwa kote nchini na baada ya kuundwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa inabidi kuhakikisha kuna utulivu wa kisiasa na amani. Na hapo kuanza juhudi za upatanishi wa watu wetu.
Mnamo vita vya miaka miwili Umoja wa Mataifa unaeleza kwamba maelfu ya watu waliuwawa kukiwa na baadhi za ripoti zikieleza kwamba hadi watu elfu 50 waliuliwa na zaidi ya milioni 2 walipoteza makazi yao.
Na katika ripoti mpya ya wafuatiliaji wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi uliyopita inawalaumu wapiganaji wa Kiir na Machar kwa mauwaji ya raia na vitendo vingine vya kikatili.
Hata hivyo Machar ametoa wito kwa jumuia ya kimataifa na viongozi wa kikanda kuendelea kuwasaidia wananchi wa Sudan Kusini kuweza kurudi katika maisha ya kawaida kutokana na athari za vita vya miaka miwili.